Siku za Mbrazili Simba zimeanza kuhesabika kwa kasi

Muktasari:

  • Tangu atue Msimbazi, Wilker ameshindwa kucheza katika kikosi cha kwanza kwa sababu ya kuwa majeruhi wa kudumu na kiwango duni alichoonyesha katika mechi alizocheza kutomridhisha Kocha Patrick Aussems

Pamoja na kusajiliwa kwa mbwembwe nyingi mwanzo wa msimu nyota wa watatu Wabrazili watatu straika Wilker Da Silva, kiungo Gerson Fraga na beki wa kati Tairone Santos siku zao zimeanza kuhesabika ndani ya Msimbazi.
Zikiwa zimesalia siku chache kabla ya kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili inaelezwa mmoja wao huenda akaonyeshwa mlango wa kutokea kurudi kwao kutokana na mabosi hao kushindwa kumsoma tangu atue kwenye kikosi chao.
Achana na Fraga aliyejitokeza kuwa kipenzi cha mashabiki wa Simba kwa aina ya soka lake na uso wake wa tabasamu muda wote. Pia mpotezee Tairone, beki ngongoti kwa sasa pale Msimbazi ambaye amekuwa akisimama sambamba na Pascal Wawa au Erasto Nyoni kwenye michezo tofauti na kuonyesha kitu flani miguuni.
Hapa tunamzungumzia Wilker, straika ambaye tangu atue Msimbazi ameshindwa kuonyesha makeke kutokana na kuwa majeruhi kila mara na hata alipokuwa fiti bado alishindwa kufanya mambo na kuwapa hofu matajiri wake waliomleta nchini, wakidhani huenda yale yaliyowakuta watani wao Yanga kwa Geilson Santana Santos ‘Jaja’ yanawakuta wao kwa straika huyo.
Jaja aliyeletwa na aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Marcio Maximo wakati akiinoa Yanga sambamba na Andrey Coutinho na kushindwa kufanya mambo akifunga mabao matatu tu, mawili kwenye mechi ya Ngao ya Jamii na jingine la Ligi kabla ya kujishtukia na kutimka akivunja mkataba wake wa miaka miwili na klabu hiyo.
Tangu atue Msimbazi, Wilker ameshindwa kucheza katika kikosi cha kwanza kwa sababu ya kuwa majeruhi wa kudumu na kiwango duni alichoonyesha katika mechi alizocheza kutomridhisha Kocha Patrick Aussems, huku pia akipata ugumu mbele ya washambuliaji wenzake waliopo ndani ya timu hiyo wanaofanya vizuri.
Mwanaspoti limepenye-zewa taarifa kuwa kwa kiwango alichokionyesha Wilker, viongozi wa timu hiyo hawajaridhishwa nacho na kwa sasa wanapanga kama wakifanikiwa kupata mchezaji wa kigeni katika dirisha dogo kama mipango yao ilivyo wanaweza kumpiga chini.
“Katika dirisha dogo tumepanga kuongeza straika mmoja, kama tutafanikiwa kumpata tutaachana na Wilker, lakini kama ikishindikana anaweza kubaki mpaka msimu ukamalizika,” alisema mmoja wa vigogo wa Simba.
Mwanaspoti linafahamu mastraika ambao Simba inawapigia hesabu ya kuwaleta ni mchezaji mpya kutoka Afrika Kusini na dili hilo linashughulikiwa na ofisa mtendaji mkuu wa timu hiyo, Senzo Mazingisa.

AUSSEMS HUYU HAPA
Kocha wa Simba, Patrick Aussems akizungumza na Mwanaspoti juu ya Wilker alikiri kikosi chake kuwa na shida ya mshambuliaji halisi kwani amekuwa akipata wakati mgumu katika mechi nyingi, akilazimika kumtumia Meddie Kagere kwa vile nahodha John Bocco ni majeruhi na Mbrazili huyo ameshindwa kuonyesha kiwango.
“Nimekuwa nikishindwa kumtumia Wilker katika mechi nyingi kutokana na kwamba hajawa fiti kimwili katika hali ya kushindana kwenye mechi zenye mahitaji ya kutumia nguvu, muda mwingi na mshambuliaji mwingine John Bocco, amekuwa akipata majeraha mara kwa mara.”
“Nadhani kama tutafanikiwa kumpata mshambuliaji asilia katika dirisha dogo litakuwa jambo muhimu katika timu, kwani Kagere anakuwa anatumika muda mwingi mwenyewe na ambaye anacheza nyuma yake muda mwingi huwa natumia viungo ambao muda mwingine wanakosa sifa za kufunga,” alisema Aussems.
“Ukiondoa shida hiyo ambayo tunayo katika safu ya ushambuliaji sioni nafasi nyingine ya kuongeza mchezaji kutokana na kuwa wengine hawajatumika kama ipasavyo kutoa mchango wao katika kuhakikisha timu inafikia malengo yake.
“Siwezi kukupa jibu la uhakika kama tutasajili au hatutasajili mshambuliaji kama ambaye tunamtaka kutokana wengi wao bado muda huu wana mikataba na timu zao, lakini kama tutafanikiwa kumpata litakuwa jambo la faida kwetu.”
Naye ofisa mtendaji wa Simba, Mazingisa, alieleza kuwa kukaa na wachezaji kwa pamoja kwa muda mrefu inasaidia kutengeneza timu imara ambayo itakuwa na ushindani katika mashindano yote, ingawa katika timu ni lazima mabadiliko yafanyike.
“Hata kama tutasajili hatutafanya usajili mkubwa kulingana na timu yetu ilivyo, nina imani ina wachezaji wazuri ambao tunaweza kumaliza Ligi Kuu Bara tukiwa mabingwa kwa mara ya tatu mfululizo na kupata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara nyingine,” alisema Mazingisa.