VIDEO: Simba, Waarabu hesabu tupu leo

Tuesday February 12 2019

By Thobias Sebastian,Charles Abel [email protected]

Dar es Salaam.Presha kubwa ya mchezo wa Simba dhidi ya Al Ahly ya Misri kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo jioni utachezwa kwa hesabu kali kulingana na msimamo wa Kundi D katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Matokeo ya ushindi kwa kila timu yatakuwa na maana kubwa zaidi katika kutengeneza mazingira mazuri ya kusonga mbele kwenye hatua inayofuata na kinyume chake yatakuwa neema kwa upande mwingine.

Kwa Simba, ushindi dhidi ya Al Ahly utaisaidia kuua ndege watatu kwa jiwe moja ambapo kwanza utaifanya kufikisha pointi sita na kuweka hai matumaini ya kufuzu hatua ya robo fainali.

Pili utaifanya iwasimamishe na kuwasogelea kwa karibu Al Ahly kwenye msimamo wa kundi hilo kwa kuwa itakuwa nyuma kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya vinara hao wenye pointi saba.

Simba ikifanikiwa katika hilo maana yake italifanya kundi kuwa wazi na kufungua milango kwa kila timu kati ya nne zinazounda Kundi D kuwa na nafasi ya kufuzu robo fainali kulingana na matokeo ya raundi mbili za mwisho zitakazobaki kwenye kundi hilo.

Pia ushindi dhidi ya Al Ahly utawafuta machozi mashabiki wake ambao hadi sasa wanaugulia maumivu ya vipigo viwili mfululizo vya mabao 5-0 walivyopata katika mechi mbili tofauti za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini dhidi ya AS Vita na Waarabu hao.

Wakati Simba ikiwa na hesabu hizo tatu, Al Ahly inalazimika kuibuka na ushindi ili kuzidi kujichimbia kileleni mwa msimamo wa kundi hilo kwa kuwa utawafanya kufikisha pointi 10.

Mbali na kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa kundi hilo, Al Ahly inaweza kufuzu rasmi katika hatua ya robo fainali iwapo AS Vita itaibuka na ushindi wa ugenini dhidi ya JS Saoura au timu hizo zikitoka sare.

Presha ya matokeo katika mchezo huo pengine ndio imefanya timu zote mbili kuonyesha wasiwasi wa kuzungumzia kwa upana maandalizi kwa ajili ya mchezo huo.

Na hilo lilijidhihirisha zaidi jana baada ya Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems kushindwa kuhudhuria mkutano baina ya timu hizo mbili na waandishi wa habari na kumtuma kocha wa makipa Mohammed Muharami ‘Shilton’ kuzungumza kwa niaba yake ingawa alizuiwa.

Hata hivyo, nahodha msaidizi Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ alitamba kuwa timu yake imejiandaa kuwashangaza Al Ahly leo licha ya kipigo cha mabao 5-0 walichopata ugenini wiki mbili zilizopita. “Siwezi kusema kocha ametupa mbinu zipi, lakini wachezaji tumejipanga kupata pointi tatu,” alisema Tshabalala.

Al Ahly kupitia kocha mkuu, Martin Lasarte ametamba kuwa wamekuwa wakifuatilia kwa karibu Simba na hawatakuwa tayari kubweteka na matokeo ya mechi iliyopita.

“Hali ya hewa ni tofauti na kwetu, lakini muda tuliofika tunajitahidi kuzoea na kufanya mazoezi katika hali hii ili kutimiza malengo. Nimepata muda wa kuwafuatilia Simba kwa kuangalia video zao na tuna imani tutaibuka na ushindi,” alitamba Lasarte.

Advertisement