Simba Mo Arena ilisubiriwa na wengi

Muktasari:

  • Wazee hao walipambana kupata eneo hilo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 19 ambapo kwa wakati huo ilielezwa kwamba bei yake ilikuwa ni Sh103 milioni ingawa katika mazungumzo ya kibiashara walipunguziwa hadi Sh91 milioni.

FEBRUARI 3, 2014 ikiwa siku ya Jumapili, wanachama wa klabu ya Simba hawatasahau moja ya kumbukumbu zao muhimu za kupigania maendeleo ya klabu hiyo.

Simba wakati huo ikiwa chini ya katibu mkuu, Ezekiel Kamwaga na msemaji akiwa Asha Muhaji walianza kampeni yao ilioitwa Operesheni Bunju ikiwa ni maalumu kwa ajili ya kuanza rasmi ujenzi wa uwanja wao.

Eneo la uwanja huo lililopo Bunju B nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam lilitafutwa na Hassan Dalali, wakati huo akiwa mwenyekiti wa klabu ya Simba na katika uongozi wake alikuwa na wenzake, Omary Gumbo (marehemu) aliyekuwa makamu mwenyekiti, Mwina Kaduguda akiwa katibu mkuu na Mohamed Mjengwa aliyekuwa katibu msaidizi na Alhams Chano (marehemu) aliyekuwa mhazini.

Wazee hao walipambana kupata eneo hilo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 19 ambapo kwa wakati huo ilielezwa kwamba bei yake ilikuwa ni Sh103 milioni ingawa katika mazungumzo ya kibiashara walipunguziwa hadi Sh91 milioni.

Oparesheni Bunju ilianza baada ya kuibuliwa kwa uwanja huo ambao ulisahaulika na wakazi wa maenezo ya huko kuvamia na kuanza kujenga nyumba zao huku sehemu zingine liligeuka kuwa malisho ya mifugo mbalimbali kama ng’ombe, mbuzi na kondoo.

Wakati wa Bunju B hawakuwa na hofu ya kujenga nyumba zao kwani hata walipohojiwa walijibu kana kwamba hawana habari kwamba eneo hilo lina mmiliki wake kwani ni kama lilikuwa limeterekezwa na Simba hivyo kila mtu aliona ana haki ya kupiga kipanda chake pale.

Lilikuwa pori hasa ambapo hata ukipita ni lazima ufikirie kukutana na nyoka ama wadudu wenye madhara makubwa kwa binadamu.

Pamoja na kutelekezwa lakini kilichovutia ni namna eneo hilo lilivyo kwamba ni tambalale lakini uongozi ulipatwa msukumo mkubwa baada ya Mwanaspoti kufichua namna eneo lao lilivyotelekezwa katika makala tatu mfululizo.

Nawapongeza viongozi hao ambao walikuwa madarakani kwa wakati huo chini ya Mwenyekiti Ismail Aden Rage na wenzake, baada ya kushtuka kuona eneo lao limevamiwa ndipo Oparesheni Bunju ilianza.

Wakiongozwa na Kamwaga safari ya wanachama hao ilianzia Makao Makuu ya Simba yaliyopo Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Saalaam saa 2 asubuhi siku hiyo ya Jumapili. Ilikuwa mwenye shoka, panga, jembe, fyekeo na kitu chochote kinachoweza kutumika kukata miti na majani makubwa eneo hilo basi walibeba na kuanza safari ya kwenda Bunju B ili kusafisha eneo lao hilo, wanachama na mashabiki wa Simba walikuwa na shauku kubwa ya kumiliki uwanja wao ndiyo maana walikubali hata kuitwa jina KILIMO KWANZA ambalo walipewa na watani zao Yanga mara baada ya kuwaona wanasafisha eneo lao.

Wakati huo mashabiki na wanachama wa Simba wanafanya yote hayo, ndani ya Simba kulikuwa na ukata kweli kweli huku upande wa watani wao wakifurahia neema waliyokuwa wakiipata kutoka kwa Mfadhili wao Yusuf Manji wakati huo, kwa ufupi Yanga hawakuwa na njaa ya pesa.

Baada ya hatua hiyo, nadhani viongozi walikaa na kujadili kwamba wafanye jambo hata kuwa na uwanja wa mazoezi tu ambapo Rage alianza kuutengeneza uwanja huo lakini muda

wake wa kukaa madaraka ulipokwisha ujenzi wa uwanja alioanzisha nao uliishia hapo hapo.

Uliingia uongozi wa Rais Evans Aveva na Makamu wake Geofrey Nyange ‘Kaburu’ pamoja na Kamati yake ya Utendaji. Mara baada ya kuchaguliwa tu jambo la kwanza ni kwenda Bunju, viongozi hao walianza ujenzi wa uwanja ukiachana na ule ambao ulianzwa na Rage. Katika hesabu zao waliweka wazi kwamba watajenga viwanja viwili, kimoja na mazoezi na kingine cha mashindano ambapo kutakuwa na uwanja wa nyasi bandia na za kawaida, kwa hakika ujenzi huo ulianza pasipo kuchelewa huku nyasi zao zikiwa zimeifika Bandarini.

Hata hivyo, viongozi hao hawakufika mbali na ujenzi wao kwani walipatwa na matatizo yaliyowaweka mikononi mwa vyombo vya dola, hivyo historia yao ya kuendeleza hilo ikaishia hapo, hawakutimiza ndoto zao kama ilivyokuwa kwa Rage ambaye aliondoka madarakani pasipo kukamilisha ujenzi ingawa alifanyakazi kubwa ya kulipia eneo hilo.

Kikubwa pia katika uongozi wa akina Aveva ni kupata hati ya eneo hilo kutoka wizara husika na mambo mengine yaliyoanza kufanywa ndani ya uongozi wao ikiwemo mabadiliko ya

mfumo wa uendeshaji kutoka klabu ya wanachama kwenda kampuni.

Baada ya mabadiliko ndipo Mwekezaji wao Mohamed Dewji ‘Mo Dewji’ walianza mchakato wa ujenzi wa viwanja hivyo viwili ambapo tayari wameanza kuvitumia kwa ajili ya mazoezi, Simba juzi Jumanne walifanya mazoezi yao kwa mara ya kwanza uwanjani hao wakitumia uwanja wa nyasi bandia.

Ni jambo kubwa ambalo limechukuwa muda mrefu huku kila kiongozi aliyepita hapo alitamani kulifanya lakini ilishindikana kwasababu mbalimbali, kikubwa tuwapongeze wote waliotafuta uwanja, waliowahi kujaribu kutengeneza uwanja na wale ambao sasa wametimiza ndoto za Wanasimba wote.