Simba SC yafunga usajili na Kichuya

JANA Jumatano mabosi wa Simba hasa Afisa Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingisa alikuwa bize kwelikweli kuhakikisha anakamilisha dili zote za usajili kabla ya saa sita usiku.

Lakini, katika dili hizo kuna moja tu ndio ilikuwa ikiwapasua kichwa nayo ni ya Shiza Kichuya, ambaye anakipiga klabu ya ENPPI ya Misri. Kwa muda mrefu Kichuya alikuwa nchini akijichimbia kule nyumbani kwao Morogoro kutokana na kile kilichoelezwa kuwa, kutokuwa kwenye wakati mzuri na klabu yake hiyo.

Awali, Simba ilimuuza Kichuya kwa dau la Dola za Kimarekani 30,000 kwenda klabu hiyo ya Misri huku akiwa kipenzi cha mashabiki wa Msimbazi.

Wakati anauzwa mapema mwaka jana, bado mashabiki wa Simba walikuwa wakiliimba jina lake kutokana na kuwapiga Yanga bao safi la kona iliyokwenda moja kwa moja nyavuni. Uwepo wake ukaishtua Simba na kuanza kumfukuzia na juzi dili la kusaini lilikwama kutokana na kutofikiwa kwa makubaliano na klabu yake hiyo ya Misri na jana ndio ukawa mshike mshike wa kuweka mambo sawa kabla ya muda kumalizika.

Mwanaspoti limezungumza na Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo ambaye amekiri kufanya mazungumzo na Kichuya na kusisitiza kwamba, wanahitaji huduma yake.

“Ni kweli tunazungumza na Kichuya ili arejee tena kuitumikia timu yake ya zamani, kuna mambo madogo ndio yametukwamisha lakini angekuwa ameishasaini mkataba tangu juzi.

“Tunapambana kuona kila kitu kinakuwa sawa hasa kumalizana na klabu yake ya ENPPI kwa kufuata taratibu zinazotakiwa,” alisema Senzo.

Ukiachana na Simba, Azam FC nayo ilianza kuzungumza na Kichuya tangu akiwa Misri ingawa hawakufikia mwafaka.

Rafiki wa karibu na Kichuya alilidokeza Mwanaspoti kwamba, Simba ilikuwa na asilimia kubwa ya kumalizana na winga huyo teleza kutokana na kuweka dau la maana mezani.

“Kichuya yupo Tanzania muda mrefu, hataki mambo yake ya usajili kuwa hadharani, lakini Simba inapambana kumrudisha nyumbani na inakaribia kufanikiwa,” alisema.

Hata hivyo, mapema jana zikaibuka taarifa kuwa mshambuliaji wa Azam FC, Shaban Idi Chilunda naye alikuwa kwenye rada za Simba.

Habari zinasema kuwa mkataba wa Chilunda na Azam umefikia tamati na kwamba, Simba walitaka kutumia nafasi hiyo kumaliza kazi.

Lakini, Senzo alipoulizwa kuhusu mkakati huo alijibu kwa kifupi: “Hapana, hakuna kitu kama hicho kwa sasa.”

SIMBA

Katika kikosi cha Simba katika dirisha dogo imeachana na straika wake Wilker Da Silva na nafasi yake kuchukuliwa na Luis Misquissone akitokea Ud Songo.

YANGA WAPYA:

Ditram Nchimbi, Yikpe Gnamien, Adeyum Saleh, Haruna Niyonzima na Tariq Seif.

WALIOTOKA:

David Molinga, Maybien Kalengo, Suleiman Moustafa na Sadney Urikhob. Pia ilitarajiwa kuwatoa kwa mkopo Ally Ally, Said Makapu na Rafael Daud.

AZAM WAPYA:

Never Tigere kutoka FC Platinumz ya Zimbambwe na Khleffin Hamdoun kutoka Mlandege Zanzibar.

WALIOTOKA:

Paul Peter kwenda Prisons.

SINGIDA UTD

WAPYA:

Athuman Idd ‘Chuji’, Haruna Moshi ‘Boban’, Ame Alli, Muharami Issa, Haji Mwinyi Mngwali, Tumba Lui na Six Mwakasega.

KAGERA SUGAR

WAPYA:

Kelvin Sabato

POLISI TANZANIA

WAPYA:

Peter Manyika Jr, Athanas Mdamu, Pius Buswita, Matheo Anthony na Jimmy Shoji.

WALIOTOKA:

Ditram Nchimbi ameondoka kwenda kujiunga na Yanga.