VIDEO: Simba SC ilivyomtuliza Minziro

Mwanza. Kocha wa Alliance Fred Felix ‘Minziro’ amesema kukosa umakini kwa wachezaji katika mchezo dhidi ya Simba, kumechangia timu hiyo kufungwa mabao 4-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Minziro alisema walianza vyema mchezo, lakini kadri muda ulivyokuwa ukisogea wachezaji walikosa umakini na kutoa fursa kwa Simba kufunga idadi kubwa ya mabao.

“Kama nilivyosema awali Simba ni klabu kubwa, tuliingia uwanjani tukiwa na game plan, lakini wachezaji wangu walipoteza umakini na kuruhusu mabao haya,”alisema Minziro.

Minziro ameanza vibaya kibarua chake baada ya kufungwa idadi kubwa ya mabao ikiwa ni mechi yake ya kwanza tangu alipopewa mikoba ya kuinoa Alliance akitokea Pamba aliyodumu muda mfupi.

Wakati Minziro akitaja sababu za kipigo hicho, kocha wa Simba Sven Vanderbroeck alisema wachezaji wake walicheza kwa kufuata maelekezo yake.

Sven alisema wachezaji walimiliki mpira na waliingia uwanjani wakiwa na matumaini ya kupata pointi tatu katika mchezo huo.

“Nina kila sababu ya kufurahia matokeo haya, wachezaji walicheza kwa umakini walifuata maelekezo na ndio sababu ya kupata ushindi,”alisema Sven raia wa Ubelgiji.

Alliance imeendelea kuwa wateja wa Simba baada ya mchezo wao wa mwisho kwenye Uwanja wa CCM Kirumba kuchapwa mabao 2-0.

Simba imeondoka Kanda ya Ziwa ikiwa na faida ya pointi sita baada ya awali kuilaza Mbao mabao 2-1 katika mchezo uliokuwa na upinzani.

Mabao ya Jonas Mkude, Meddie Kagere, Clatous Chama na Hassan Dilunga yalitosha kuipa Simba pointi tatu na kufikisha 41.

Kuingia bao la pili kuliwafanya wachezaji wa Alliance kutoka mchezoni na kuanza kucheza faulo mara kwa mara wachezaji wa Simba ambazo ziliwagharimu.

Simba ilitumia udhaifu huo kupitisha mipira ya pembeni kwa mabeki Shomari Kapombe na Mohammed Husssein ambao walipiga krosi nyingi.

Mchezo wenyewe

Awali, dakika ya 12 Dilunga alikosa bao baada ya kiki yake kudakwa na kipa wa Alliance John Mwanda, kabla ya Sharaf Shiboub kukosa dakika ya 19.

Alliance ilifanya shambulizi la kushitukiza kupitia kwa Chinedu Michael kabla ya dakika ya 27 Israel Patrick kufunga bao.

Patrick alifunga bao kwa mpira wa faulo kufuatia Erasto Nyoni kumuangusha David Richard nje ya eneo la hatari ambapo kiki yake ilimpita kipa wa Simba Beno Kakolanya.

Simba ilipa bao kupitia kwa Mkude aliyefungua kwa shuti lilloenda moja kwa moja wavuni na kumuacha kipa Mwenda akiwa ameduwaa.

Dakika ya 59 Kagere alifunga bao la pili Simba akiunganisha mpira wa kichwa wa Shiboub kabla ya dakika 63 Chama kuongeza la tatu kwa mpira wa faulo. Dilunga alifunga bao la nne dakika ya 72.

Alliance: John Mwanda, Israel Patrick, Makenzi Ramadhani, Geofrey Luseke, Eric Mrilo, Martin Kigi, Juma Nyangi, Michael Chinedu, David Richard na Siraji Juma.

Simba:Beno Kakolanya, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Clatous Chama, Sharaf Shiboub, Meddie Kagere, Hassan Dilunga na Francis Kahata.