Simba bana dakika 450 Sh 2 Billioni

Friday March 22 2019

 

By THOBIAS SEBASTIAN

WAWAKILISHI wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba mara baada ya kufuzu katika hatua ya makundi ni kama wanakoga pesa wakati huu kutokana na vyanzo vya pesa ambavyo watavipata sehemu mbalimbali.

Simba wamefuzu katika hatua ya makundi wakianzia katika hatua ya awali baada ya kuzitoa timu ya Mbabane Swallows ambao waliondolewa kwa jumla ya mabao 8-1, na Nkana Red Devils ya Zambia walitolewa kwa jumla ya mabao 4-3.

Baada ya hapo walikwenda hatua ya makundi na walipangwa kundi ‘D’ na Al Ahly, As Vita na JS Saoura.

Katika mashindano Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ngazi ya klabu Shirikisho la Soka Afrika (CAF), huwa linatoa Dola 550,000 kwa timu yoyote ambayo imefuzu hatua ya makundi na kumaliza katika nafasi ya tatu au nne.

Timu ambayo itamaliza katika nafasi ya kwanza au ya pili pesa hiyo itaongezeka na kufikia Dola 650,000 ambayo ukiibadilisha kwa pesa ya Kitanzania unapata zaidi ya Sh1.5 bilioni.

Kwa maana hiyo, Simba wamefuzu katika hatua ya robo fainali watavuta pesa hiyo ambayo itaingia katika akaunti yao kwa vipindi tofauti.

Advertisement

Simba mbali ya kuvuta mkwanja huo kutoka CAF, watapata bonansi nyingine ya pesa kutoka kwa wazamini wao wa SporpPesa ambao huwa wanawapa mkwanja kila timu hiyo inapofanya vizuri katika mashindano mengine.

Ofisa mtendaji mkuu wa Simba, Crescentius Magori alisema wadhamini wao SportPesa watawapa Sh 50, millioni ambayo ni bonasi ya pesa ambayo inapatikana katika mkataba wao ambao waliingia wa miaka mitano.

Magori alisema kuna sehemu ya mkataba ambayo inaonyesha kuna kiasi cha Sh50, milioni ambacho tutapata kutoka kwa wadhamini wetu baada ya kuingia hatua ya robo fainali ya mashindano haya.

“Hii pesa ni kama motisha ya kutuongezea kufanya vizuri kwa wachezaji wetu ili katika mashindano haya na kuendelea kuwatangaza kila ambavyo tutakuwa tunafika mbali,” alisema.

“Motisha hii si katika Ligi ya Mabingwa tu bali hata tukifanya vizuri kama kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara na mashindano mengine wanatupatia na hilo tukiri kwetu mpaka kwa wachezaji linaongeza hali ya kushindana,” alisema Magori.

Wawakilishi hao wa Tanzania wameendelea kuvuna zaidi mkwanja katika mechi zao tano ambazo wamecheza katika ardhi ya nyumbani, mbili zikiwa katika hatua ya awali na tatu kwenye makundi.

Simba katika hatua ya awali walicheza na Mbabane Swallows na Nkana Red Devils huku katika hatua ya makundi walicheza tatu nyumbani na JS Saoura, Al Ahly na As Vita.

Katika mechi ya As Vita mapato yaliyopatikana mlangoni Sh150, milioni ambayo mpaka inakatwa makato yote Simba walichukua Sh70, milioni.

Katika mechi na Al Ahly walipata jumla Sh120, milioni na wao mpaka wanapewa ilikuwa Sh50 milioni.

Katika mechi na Nkana walishinda mabao 3-1, na kupata nafasi ya kusonga mbele katika hatua ya makundi huku mashabiki ambao walijitokeza kushuhudia mechi hiyo waliingiza zaidi ya Sh165, milioni kama mapato ya mlangoni ambacho kilipatikana mara baada ya mechi kumalizika.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba Mulamu Ng’ambi alisema katika mechi hiyo dhidi ya Nkana ilipatikana zaidi ya Sh165 milioni kabla ya kwenda katika makato kama ya uwanja na sehemu nyingine husika.

“Nadhani baada ya makato yote tulipata si chini ya Sh60 milioni ambayo kwetu ilitusukuma kuongeza nguvu kupata uwanja wetu hata wa mazoezi kwani makato huwa yanaumiza katika klabu zetu hizi,” alisema Ng’ambi.

Mabosi wa Simba katika kuhakikisha wanapata mkwanja katika viingilio kwenye mechi ya JS Saoura waliweka tiketi za Platinamu ambazo zilikuwa zinauzwa kwa Sh100,000 ambazo kwa yoyote aliyefanikiwa kukata alitakiwa kwenda hoteli ya Serena na walichukuliwa na mabasi maalumu ambayo yaliwapeleka uwanjani na kuwarudisha hoteli mpira ulipoisha huku wakisindikizwa na msafara wa polisi.

Tiketi za Platinamu ambazo Simba waliziuza zilikuwa 120, ambapo waliweza kukusanya Sh12 milioni huku mashabiki waliokata tiketi hizo walipata huduma ya kunywa na kula muda wote walipokuwa uwanjani na kila mmoja alipewa jezi ya Simba.

Simba mbali ya kupata Sh12, milioni katika tiketi 120, za Platinamu walikusanya Sh195, milioni kama mapato ambayo yalipatikana mlangoni kwa mashabiki wote waliongea uwanjani mbali ya wale ambao walikuwa na tiketi za Platinamu. Katika mechi dhidi ya Mbabane Swallows baada ya makato yote Simba walipata Sh73 milioni. Kwa haraka ni kwamba, Simba inaweza kuwa imevuna Sh 2 bilioni.

WASIKIE SIMBA WENYEWE

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema hayo ndio mapato ambayo waliyapata katika mechi tano ambazo wamecheza nyumbani lakini inaonekana makato yamekuwa mengi ndio maana wanapata pesa nusu ya ile yote.

“Mashabiki walijitokeza kwa wingi katika mechi zetu za nyumbani tunashukuru hilo lakini hili la makato nadhani linaweza kutazamwa upya ili kuzipa nguvu klabu katika pesa ambazo zinapatikana milangoni,” alisema Try Again.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Mulamu Ng’ambi alisema pesa za CAF, zinaingia kwa mafungu lakini malengo makubwa ni kutumika katika mahitaji muhimu haswa timu kucheza katika mechi inayifata.

Ng’ambi alisema unajua hawa CAF, huwa wanatoa pesa hizo ili kusaidia timu kuweza kusafiri kwenda kucheza mechi katika nchi nyingine na gharama nyingine za msingi ambazo zitawezesha timu husika kuishi bila shaka.

“Tukizipata pesa hizi huwa zinapunguza gharama kama za hoteli, usafiri na mambo mengine yote ya msingi na zile ambazo tulibidi tupokee za kwanza tayari CAF, wameshatuwekea za awamu ya kwanza,” alisema.

Advertisement