Simba itapenya hapa kwa AS Vita

Muktasari:

  • Simba itacheza na AS Vita ukiwa ni mchezo wa mwisho kwa timu hizo katika kundi lao

Dar es Salaam. Sababu tatu zinaifanya Simba iwe katika nafasi nzuri ya kuibuka na ushindi kwenye mchezo muhimu wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita Club ya DR Congo.

Simba na AS Vita zinatarajiwa kumenyana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kesho. Mchezo wa kwanza AS Vita ilishinda mabao 5-0.

Kiwango na matokeo yasiyoridhisha ya AS Vita inapokuwa ugenini, ubora, rekodi inayovutia ya Simba inapocheza nyumbani na hamasa ya mashabiki vinaiweka Simba katika nafasi nzuri kisaikolojia.

Pamoja na kutambulika kama moja ya timu tishio katika mashindano ya klabu Afrika, Vita haichezi vizuri na haina matokeo mazuri ugenini, rekodi inayoweza kuwapa hofu na kuwafanya wacheze kwa presha katika mechi hiyo jambo ambalo linaweza kuwa na faida kwa Simba.

Mechi 10 za mwisho ambazo Vita ilicheza ugenini katika mashindano ya klabu Afrika, imepata ushindi mara moja tu, ilitoka sare mechi nne na kupoteza michezo mitano. Imefunga mabao manane na kufungwa 13.

Kudhihirisha Vita haina kiwango ugenini, katika mechi tano zilizopita, safu yake ya ushambuliaji imefunga bao moja tu ilipotoka sare ya bao 1-1 na Bantu FC ya Lesotho.

Vita inakutana na Simba ambayo ni tishio inapocheza nyumbani na kuthibitisha hilo, katika michezo 10 ya mwisho ya mashindano ya klabu Afrika, imeibuka na ushindi mara nane.

Pia imetoka sare moja, kufungwa moja, wakipachika mabao 24 ikiwa ni wastani wa mabao mawili kwa kila mchezo huku wakifungwa mabao sita tu.

Mechi moja ambayo Simba ilipoteza miaka sita iliyopita ilifungwa na Recreativo Do Libolo ya Angola iliyoshinda bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Februari 17, 2013.

“Hii ni mechi ya fainali kwetu na kwao, siamini kama rekodi za kufanya vibaya kwa Vita ugenini au sisi kutamba nyumbani zinaweza kuwa na nafasi. Jambo la muhimu ni wachezaji kucheza kwa kujitolea waitumie vizuri nafasi hii kuandika historia kwao, klabu na Taifa lao,” alisema Kocha Patrick Aussems.

Hofu kubwa kwa Simba ni kukosekana kwa nyota wawili muhimu wa kikosi cha kwanza ambao ni Juuko Murshid aliye majeruhi na Jonas Mkude anayetumikia adhabu ya kadi.