VIDEO: Simba itawakosa Bocco, Mkude, Kapombe ikiivaa Azam katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania

Muktasari:

  • Katika mchezo huo Simba inaingia ikiwa vinara wa ligi baada ya kukusanya pointi 12, katika michezo minne wakati Azam imekusanya pointi tisa katika mechi tatu huku timu zote mbili zikiwa hazijapoteza mchezo wowote.

Dar es Salaam. Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba bila ya nyota wake wanne Mohammed Hussein 'Tshabalala', John Bocco, Jonas Mkude na Shomari Kapombe itaivaa Azam kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wachezaji hao jana walishindwa kufanya mazoezi na wenzao jioni hivyo kunauwezekano mkubwa wakakosekana katika mchezo huo.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema Tshabalala aliumia akiwa na Taifa Stars alitakiwa kwenda hospitali, Mkude ameumia kidole gumba akiwa na Taifa Stars wakati Kapombe ameshindwa kufanya mazoezi kutokana mwili wake haupo sawa ila Bocco ndio ametoka majeruhi hawezi kuwa fiti.

"Wote wanaendelea na matibabu na bado tunasiku moja ya leo Jumatano kama wataweza kutumika au hawateweza hilo litafahamika na benchi la ufundi wao ndio wataamua mbadala wa kucheza katika nafasi zao," alisema Rweyemamu.

Katika mchezo huo Simba inaingia ikiwa vinara wa ligi baada ya kukusanya pointi 12, katika michezo minne wakati Azam imekusanya pointi tisa katika mechi tatu na timu zote mbili hakuna iliyopoteza hata mchezo mmoja.

Akizungumzia mchezo huo kocha wa Simba, Patrick Aussems alisema katika akili yao benchi la ufundi pamoja na wachezaji si wakati wa kuangalia rekodi za nyuma walipata matokeo mazuri dhidi ya Azam au walitoka kufanya vizuri katika michezo mitatu ya kirafiki bali wanafanya maandalizi ya kutosha ili waweze kushinda mchezo huo.

"Nadhani ni wakati sahihi wa kuangalia haya maandalizi tunafanya wakati huu kuliko kuangali rekodi yetu nzuri dhidi ya Azam," alisema.

"Tunakwenda kucheza na timu yenye wachezaji wazuri ndio maana tumefanya mazoezi ya kucheza hapa na yenye mbinu nyingi ndani yake ambayo tutakwenda kuyatumia katika mchezo huo wa kimashindano na tunafanya hivi lengo letu ikiwa ni kupata pointi tatu," alisema Aussems.

Kocha msaidizi wa Azam, Idd Nassor 'Cheche' alisema hautakuwa mchezo rahisi kutokana wanakwenda kucheza na timu kubwa iliyokuwa na wachezaji wazuri.

"Kila timu imefanya maandalizi ya kutosha ndio watakuwa na nafasi ya kwenda kupata ushindi katika mechi ya leo jioni, lakini kwa upande wetu kila kitu kimekwnda sawa na tunasubiri wachezaji waende kutekeleza kile ambacho tumefanya mazoezini," alisema Cheche.