Simba kicheko, Azam, Mtibwa zapasuka

BAO pekee lililofungwa na Nahodha wa Simba, John Bocco limeiwezesha timu hiyo kujiimarisha zaidi kileleni wakifikisha pointi 56 baada ya kuibuka na ushindi mbele ya wenyeji wao Lipuli FC.
Mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara imechezwa Uwanja wa Samora mjini hapa ambapo Simba imeshinda bao 1-0 ambapo Bocco alifunga bao hilo dakika ya 23.
Wakati Simba ikishangilia ushingi huko Iringa, vigogo Azam, Mtibwa Sugar wao wameambulia kichapo kwenye mechi zao za leo Jumamosi.
Azam ilikuwa Uwanja wa Uhuru dhidi ya Coastal Union ambapo wameambulia kipigo cha bao 2-1 huku Mtibwa Sugar wao wakipokea kipigo nyumbani dhidi ya JKT Tanzania bao 1-0, mechi imechezwa Uwanja wa CCM Gairo, Morogoro.
Yanga yenyewe itakuwa na kibarua leo saa 1 usiku dhidi ya Prisons mechi itakayochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Singida United na Mbeya City mazingira yao yanaendelea kuwa magumu kutokana na matokeo yao kuendelea kuwa mabaya ambapo mechi za leo wamepoteza, MCC imefungwa ugenini bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting wakati Singida yenyewe imepoteza nyumbani bao 1-0.
Kwa upande wa KMC nayo mambo si mazuri baada ya leo kupokea kichapo kutoka kwa maafande wa Polisi Tanzania bao 3-2 huku Mwadui na Namungo zikitoka sare ya bao moja wakati Biashara yenyewe ikitakata nyumbani dhidi ya Alliance bao 1-0.
Kagera Sugar ikiwa nyumbani Uwanja wa Kaitaba imeshinda bao 2-0 dhidi ya Mbao FC.