Simba inapenyea hapa kwa TP Mazembe

Muktasari:

  • Timu ambazo zimeingia robo fainali pamoja na Simba ni Al Ahly ya Misri, Wydady Casablanca ya Morocco,  TP Mazembe ya Congo, CS Constantine ya Algeria, Horoya ya Guinea na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Droo ya CAF ya Ligi ya Mabingwa Afrika imepangwa leo Jumatano nchini Misri na wawakilishi pekee wa Tanzania, Wekundu wa Msimbazi Simba watacheza na TP Mazembe katika hatua hiyo na wataanzia nyumbani.
Simba imefuzu robo fainali ikitokea Kundi D pamoja na Al Ahly iliyopangiwa kucheza na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika hatua hiyo na kuziacha AS Vita ya Congo na JS Saoura ambazo zitabaki kuwa watazamaji.
Wekundu hao wataanzia nyumbani mchezo utakaopigwa kati ya  Aprili 5-6, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na mechi ya marudiano itapigwa Lubumbashi, Congo kati ya Aprili 12-13.
Droo hiyo iliyochezeshwa mbele ya wawakilishi wa Simba, Mtendaji Mkuu, Crescentus Magori na Mwenyekiti Swedi Nkwabi na ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu na mashabiki pamoja na wadau wa soka Afrika kwa jumla.
Simba inacheza na TP Mazembe ambayo walikutana nayo kwa mara ya mwisho mwaka 2012 katika mashindano hayo. Katika mchezo huo, Simba walifungwa lakini walipata nafasi ya kusonga mbele baada ya TP Mazembe kukutwa na makosa ya kumchezesha mchezaji asiye na sifa.

Ratiba kamili
CS Constantine ya Algeria VS Esperance de Tunis ya Tunisia
Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini VS Al Ahly ya Misri
Horoya ya Guinea VS Wydady Casablanca ya Morocco
Simba ya Tanzania VS TP Mazembe ya Congo