Ratiba ya CAF: Simba kwa UD Songo, Yanga yatupwa kwa Rollers

Muktasari:

  • Kwa mara ya kwanza Tanzania imekuwa na timu nne katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Afrika (CAF), lilitangaza ratiba ya mechi za awali za mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika, ikionyesha mabingwa Ligi Kuu Bara, Simba ikianza ugenini dhidi UD Songo ya Msumbiji, huku Yanga ikirudishwa kwa Township Rollers ya Botswana.

Simba pamoja na kufanikiwa kufuzu kwa robo fainali msimu uliopita itaanzia hatua ya awali kwa kucheza mechi ugenini dhidi ya UD Songo katika mechi itakayochezwa kati ya Agosti 9-11 na marudiano itakuwa kati ya Agosti 23-25, 2019.

Mshindi wa mechi ya Simba na UD Songo atasonga mbele na kucheza dhidi ya mshindi wa mechi ya Big Bullets na FC Platinum kati ya Septemba 13-15, 2019 na marudiano Septemba 27-29, 2019.

Katika ratiba hiyo Yanga itaanzia nyumbani kwa kucheza dhidi ya Township Rollers timu waliyokutana nayo mwaka 2018 katika michuano hiyo na Vijana wa Jangwani kutolewa kwa kufungwa jumla ya mabao 2-1, ikilala nyumbani kwa bao hizo na kwenda kutoka suluhu ugenini.

Mshindi wa Yanga na Township Rollers atafuzu kwa raundi ya pili na kucheza na mshindi wa mechi kati ya Green Mamba ya eSwatini au Zesco United ya Zambia. Mshindi wa mechi hizo za pili inafuzu moja kwa moja kwa hatua ya makundi ya mashindano.

Katika Kombe la Shirikisho Afrika, mabingwa wa Kombe la FA, Azam itaanza ugenini dhidi ya Fasil Kenema ya Ethiopia kati ya Agosti 9-11, 2019.

Mshindi wa Azam dhidi ya Fasil Kenema atacheza na mshindi wa mechi kati ya Triangle United (Zimbabwe) dhidi ya Rukinzo (Burundi) katika raundi ya pili.

KMC inashiriki kwa mara ya kwanza mashindano hayo ikiwa chini ya kocha Jackson Mayanja itakuwa nyumbani kuikaribisha AS Kigali (Rwanda) anayoichezea Haruna Niyonzima aliyeachwa na Simba msimu huu.

Mshindi wa KMC na AS Kigali atacheza na mshindi wa mechi ya Proline (Uganda) dhidi ya Masters Security (Malawi)