Simba na Yanga, bampa kwa bampa

Muktasari:

Ndani ya dakika 29 Simba wameweza kupata kona mbili, huku Yanga wakiwa hawajapata kona yoyote.

Dar es Salaam. Mchezo wa Yanga na Simba umegeuka kuwa mchezo wa ubabe, kuliko kutumia mbinu za ufundi katika dakika 45 za kwanza zimemalizika kwa suluhu.

Katika mchezo huo Simba walikuwa wakitumia zaidi uoande wa kulia uliokuwa ukichezwa na beki Zana Coulibaly, ambaye alionekana kuwa na uharaka katika kupeleka mashambulizi na kupiga krosi.

Kwa upande wa Yanga wao walionekana kukaba zaidi kutokana na kutokuwa na mipango dhabiti ya kushambulia tofauti na kwa upande wa Simba.

Dakika 6 Simba walipata kona baada ya Gadiel Michael kuutoa mpira, hata hivyo kona hiyo iliyopigwa na Emmanuel Okwi haikuwa na faida.

Yanga waliamka na kuamua kutumia mipira mirefu katika kupeleka mashambulizi, staili hiyo ilionekana kwao bora kutokana na kushindwa kuweka mipira chini.

Dakika 7 Paul Godfrey alianzishiwa pasi fupi na Ibrahim Ajib, alipiga shuti kali na kupaa pembezoni mwa mwamba wa juu.

Simba walizidi kushambulia zaidi lakini walikuwa hawawezi kupita katikati ya mabeki Andrew Vicent na Kelvin Yondani.

Dakika 17 Simba walipata kona nyingine lakini hata hivyo umakini wa Simba ulikuwa mdogo na kushindwa kufanya vizuri katika kona hizo mbili walizopata.

Beki Paul Godfrey dakika 23 alipanda kwa spidi na mpira lakini beki wa Simba,Mohammed Hussein alimfanyia madhambi na kaudhibiwa kwa kupewa kadi ya njano.

Faulo fupi iliyopigwa na Ibrahim Ajib, ilitaka kuzaa bao hata hivyo umakini wa Andrew Vicent ulikuwa mdogo na kushindwa kuipa bao Yanga.

Yanga walionekana kufunguka baada ya kucheza takribani dakika 24 bila kushambulia, dakika 25 walikosa goli baada ya Ajib kumpigia Makambo pasi mpenyezo na kuunganisha lakini hata hivyo ulipaa juu kidogo ya goli.

Ndani ya dakika 33 za mchezo huu, Simba walionekana kuwa watulivu zaidi kuliko Yanga kwenye kuhakikisha wanapeleka mashambulizi.