Simba na Yanga ni nje tu; ndani kugumu

Muktasari:

  • Nakumbuka kwamba wakati nilipokuwa Katibu Mkuu wa Simba, klabu ilikuwa na mdhamini ambaye ni bia ya Kilimanjaro. Wakati naanza, udhamini ulikuwa umefikia takribani Sh 30 milioni.

NINAMFAHAMU vyema Mwenyekiti wa Yanga, Profesa Mshindo Msolla kama mwanamichezo na kama mwanataaluma. Ni mtu mtulivu, mwenye akili na asiyekurupuka kwenye mambo yake.

Nilikuwa mmoja wa watu waliofurahi wakati alipopata nafasi ya kuwa mwenyekiti wa Yanga. Kwa muda mrefu, mimi nimekuwa mmoja wa watu wanaoamini kwamba kuna viongozi wa soka nchini ambao wamekaa kwa muda mrefu kiasi kwamba wanahusika na karibu kila aina ya ubabaishaji unaoliandama soka la Tanzania.

Bado naamini kwamba ni mtu sahihi kuongoza Yanga katika kipindi hiki cha mpito wakati wanatafuta mwekezaji wa maana kama ambavyo Simba imefanikiwa kumpata Mohamed Dewji ‘Mo’.

Kuna vitu vingi katika klabu hizi ambazo mtu aliye nje hawezi kujua mpaka atapoingia ndani na kuwa sehemu ya uongozi.

Nilibahatika kuwa mmoja wa viongozi wa klabu ya Simba miaka kadhaa nyuma. Kile ambacho Yanga ya Msolla inakipitia sasa ninakielewa kwa sababu wakati wangu tatizo lilikuwa lilelile na kama mfumo hautabadilika, tatizo halitaondoka leo wala kesho.

Nakumbuka kwamba wakati nilipokuwa Katibu Mkuu wa Simba, klabu ilikuwa na mdhamini ambaye ni bia ya Kilimanjaro. Wakati naanza, udhamini ulikuwa umefikia takribani Sh 30 milioni.

Hata hivyo, nilikuja kubaini baadaye kwamba mishahara ya wachezaji pekee ilikuwa imefikia takribani Sh 55 milioni.

Maana yake ni kwamba kila mwezi klabu ilikuwa na upungufu wa walau Sh 25 milioni kulipa mishahara pekee. Ikumbukwe kwamba klabu ilikuwa na utamaduni wa kuweka wachezaji kambini kwa sehemu kubwa ya mwaka na gharama zake ilikuwa walau Sh 1 milioni kwa siku.

Kwa sababu klabu haikuwa na uwanja, kulikuwa na gharama za kulipia viwanja kila siku na kama wachezaji wanatokea majumbani mwao, kulikuwa na posho ya nauli kwa wachezaji na benchi la ufundi waliokuwa wakija mazoezini.

Kama timu inafanya vizuri, mashabiki watakuja viwanjani na pesa, kupitia mapato ya mlangoni itajazia kwenye akiba ya klabu. Lakini kama timu haifanyi vema kama ilivyokuwa Simba wakati wangu; dhidi ya Yanga ya Yusuf Manji na Azam FC ya Yusuf Bakhresa, mashabiki wanakata mguu kwenda uwanjani.Na kuna ule wakati ambao ligi imesimama na hakuna mechi za kucheza. Ndipo sasa unapoona pengo kubwa baina ya mapato na matumizi. Na kwa sababu kwa muda mrefu klabu hivi havikuwa na utamaduni wa kulipa kodi wala mambo mengine ya kisheria, ulipoingia utaratibu huu timu hizi kubwa zilijikuta zimeingia kwenye madeni makubwa.

Kuna tatizo lingine la watu wanaoitwa wafadhili ambao huziingiza klabu hizi kwenye hasara kubwa kwa kusajili wachezaji kwa gharama kubwa pasipo kuzingatia uwezo wa klabu kulipa gharama hizo.

Mfano mmoja naukumbuka sana. Kuna wakati mmoja wafadhili wa klabu waliamua kumsajili mchezaji mmoja kwa gharama ya mamilioni ya shilingi lakini nilipoulizia habari zake niliambiwa ni mchezaji ambaye atakuwa msumbufu kwa klabu kwa sababu alikuwa amejiingiza katika ulevi wa kila aina ya kilevi.

Tajiri alilazimisha mchezaji huyo asajiliwe. Alisajiliwa na deni likaingia klabu. Kimsingi, tabia ambazo vigogo hawa wanazifanya kwenye biashara zao ni tabia tofauti na wanavyotaka klabu ziendeshwe.

Hawawezi kuruhusu kampuni zao zitumie zaidi ya zinachoingiza lakini ziko tayari kuona klabu zinatumia zaidi ya kinachoingia. Na bado kuna matumizi mengine chungu nzima ambayo hayaandikiki gazetini lakini ni sehemu ya matumizi muhimu kwa klabu zetu.

Siri kubwa ya kuzifanya klabu hizi zijijenge zaidi ni kwenye kuhakikisha matumizi yanaenda sawa na mapato na hili ni jambo ambalo linaweza kufanywa na watu kama Msolla ambao hawana makandokando na mfumo huu mbovu ambao umejengwa kwa muda mrefu.

Ni rahisi sana kuwalaumu viongozi wa hivi klabu lakini kama watu wangekuwa wanajua nini kinachoendelea ndani, pengine wangeelewa nini hasa kinatakiwa kufanywa.

Kuna kazi ya kuongeza mapato zaidi lakini kuna namna ya kutumia kile kidogo kilichopo vizuri. Hii ndiyo changamoto ambayo Msolla, Frederick Mwakalebela ambaye ni Makamu wake na wenzao wanatakiwa kuifanyia kazi.

Wanafundishika?

Wikiendi iliyopita, Jose Mourinho, alizungumza jambo ambalo limenifikirisha kidogo. Akizungumzia bao lililofungwa na Son Heung Min, Mourinho alisema mchezaji huyo kutoka Korea Kusini ni wa aina yake na akazungumzia utamaduni wa Wakorea kwamba ni watu ‘wanaofundishika’.

Maneno hayo ya Mourinho yamenifundisha jambo moja muhimu; kwamba kuna watu ambao kwa utamaduni wao ni watu ambao ni rahisi kupokea mafunzo yoyote na hivyo wanafundishika.

Maana iliyojificha katika maelezo ya mwalimu huyo wa Tottenham Hotspurs ni kwamba wapo wachezaji ambao kiutamaduni kwao ni vigumu sana kufundishika.

Kwamba wapo wachezaji ambao ukitaka wawe wazuri inabidi urahisishe mafunzo yako. Ukimpa taarifa nyingi inakuwa sawa na ule mkasa wa mbwa ambaye amepotezwa na miluzi mingi. Taarifa kidogo tu na mchezaji anakuwa mzuri.

Hili ni jambo ambalo walimu wetu wa soka na michezo mingine wanatakiwa kulifahamu. Wachezaji hawafanani. Na hii, kwa mtazamo wangu, ni muhimu sana kwa makocha wa Tanzania kuliko hata Ulaya kwa sababu wengi wa wachezaji wetu hawajapata elimu ya darasani kwa kiasi cha kutosha.

Mtu ambaye amewahi kukaa darasani kwa miaka miwili tu –tena kwa mbinde kwelikweli, unamchanganya tu ukiamua kumwelewesha kwa kutumia ma Ipad na picha za video za kutosha. Maelezo madogo tu ya nini cha kufanya na mambo yanakuwa murua kabisa. Hili ni somo muhimu sana kulielewa.