Simba wamelamba dume kumsajili Mwamnyeto

WAKATI Simba ikitajwa kumalizana na beki wa kati wa Coastal Union, Bakari Mwamnyeto, kiungo wa zamani wa Polisi Mara, Musa Keita amesema Wekundu hao wa Msimbazi watakuwa wamelamba dume kumsajili nyota huyo kwani wataboresha safu yao ya ulinzi ambayo kwa sasa haiko sawa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Keita alisema amekuwa akimfuatilia beki huyo katika mechi mbalimbali za Ligi Kuu alizocheza msimu huu na kugundua ni moja ya mabeki wazuri ambao kama wakitua Simba ataweza kuimarisha safu ya ulinzi.

Alisema Mwamnyeto yuko vizuri katika ukabaji na pia muda wote yuko makini uwanjani pamoja na kuwa na nidhamu ya mchezo ambayo wachezaji wengi hasa mabeki huwa mara nyingi hawana.

“Msimu huu nimemfatilia katika mechi zaidi ya 10 nikaona ni moja ya mabeki wa kati wazuri kwenye Ligi Kuu kwanza anacheza kwa kujituma na pia ana nidhamu kubwa uwanjani ambayo inamsaidia sana wakati wa kudhibiti mashambulizi,” alisema Keita.

Keita alisema kwa sasa Simba ilikuwa inahitaji beki wa kati ambaye ataweza kuimarisha safu yao ya ulinzi ambayo katika mechi za msimu huu imekuwa haiko katika ubora unaotakiwa.

“Unajua Simba msimu huu imekuwa na beki mbovu sana lazima tuseme ukweli angalia mabao wanayofungwa ni mepesi sana kikubwa wanatakiwa kufanya usajili makini kwenye eneo la ulinzi ambao utawasaidia msimu ujao,” alisema kiungo huyo.