Simba yafanya kufuru Congo

UKISIKIA jeuri ya feda ndio hii, ambayo inaonyeshwa na Simba pale kwenye ardhi ya Jiji la Kinshasa nchini DR Congo. Simba imetua jana Alhamisi jijini humo na kupokewa kishujaa huku Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania, ukisimamia shoo nzima kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri.

Kesho Jumamosi jeshi hilo la Kocha, Patrick Aussmes litakuwa uwanjani kukipiga na wenyeji wao, AS Vita kwenye mechi yake ya pili hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo msafara wake umetua mjini hapa ukiwa na kikosi cha wachezaji 19 na wataalamu wa benchi la ufundi.

Mbali na kikosi hicho pia Mkurugenzi Mtendaji Crescentius Magori akiongoza msafara huo pamoja na Katibu wa klabu Dr. Arnold Kashembe.

Hapa Mwanaspoti ambalo kama kawaida limeweka kambi jijini Kinshasa kwa ajili ya kukuletea kila kinachojiri kabla na baada ya mchezo huo.

Kambi sio mchezo

Kwa sasa hali ya usalama nchini hapa sio kama ile ambayo tumekuwa nayo kule Tanzania, DR Congo mambo hayajatulia kutokana na mvutano wa matokeo ya uchaguzi ambao umemalizika hivi karibuni. Kwa kutambua hilo na hali halisi iliyopo, taratibu zote kuhusiana na usalama wa kikosi cha Simba ziko vizuri na Ofisi ya Ubalozi ndio inaratibu kila kitu.

Kikosi cha Simba kimeweka kambi kwenye hoteli ya kifahari yenye hadhi ya nyota tano ya Pullman Grand Hotel. Hoteli hiyo ambayo ni maarufu jijini hapa, iko kwenye mandhari mazuri na tulivu huku ikiwa na huduma zote muhimu ambazo zitaongeza utulivu kwa wachezaji.

Kuna mabwawa ya kutosha ya kuogelea na vyumba vyenye kila kitu ndani, japo wachezaji na viongozi wa Simba watakosa huduma za mitandao ya kijamii kama wanapokuwa nchini Tanzania. Kwa sasa hapa DR Congo, huduma za mitandao yote ya kijamii kama WhatsApp, Twitter, Instagram na Facebook, zimefungiwa kutokana na vuguvugu la uchaguzi huo hivyo, ndio kitu pekee ambacho watakimiss.

Wapangua hujuma

Kama kuna mabosi wenye mipango na wanaojua kupangua fitina za wapinzani basi ni hawa wa Simba. Fitina na hujuma walizokutana nazo huku sio za kitoto, lakini mapema kabisa waligundua kila kitu na kuweka mikakati mbadala.

Awali, mabosi wa Simba walikuwa wakiendesha mambo kimya kimya ikiwemo mahali ambako wataweka kambi kubaki kuwa siri hadi jana walipotua jijini hapa.

Hata hivyo, ghafla tu baada ya kikosi kufika wakashtukia jambo kuwa wapinzani wao wameweka mtego mpya na kufanya uamuzi mgumu wa kupanga kuhama hotelini hapo.

“Timu imefika salama na kila kitu kinakwenda vizuri, usalama upo wa kutosha na timu ipo kwenye mikono salama ya Ubalozi wetu nchini hapa, tunaangalia uwezekano wa kuhama kutoka hapa tulipo kwa sababu kuna jambo tumeona haliko sawa kidogo. Hata hivyo, tutashauriana zaidi kama tutaweza kulidhibiti tutaendelea kuwepo hapa,” alisema Salim Abdallah ‘Try Again’.

NIYONZIMA, DILUNGA WAMVURUGA AUSSEMS

Lakini, wakati kikosi cha Simba ambacho kilianza vyema kampeni yake kwenye hatua hii kwa ushindi wa kishindo wa mabao 3-0 JS Saoura, kikijiandaa kushuka dimbani, Aussems ameanza kuvurugwa kidogo na mastaa wake.

Iko hivi. Aussems tayari ameweka mipango na mikakati ya kikosi chake cha kwanza ambacho kitaanza katika mechi ya kesho, ambako nahodha wake, John Bocco, hatakuwepo na huenda akabadili mfumo mzima wa uchezaji. Pia, beki Erasto Nyoni ambaye aliukosa mchezo wa kwanza dhidi ya JSS, pengo lake lilishapata mzibaji tena wa kibabe, Juuko Murushid.

Kikosi cha Simba chini ya Aussems tangu kimeanza kucheza mechi za kimataifa katika mechi moja tu dhidi ya JS Saoura, ndio alianza na washambuliaji wawili Bocco na Emmanuel Okwi, lakini zingine amekuwa akianza na washambuliaji watatu.

Katika kuhakikisha pengo hilo la Bocco linazibwa katika mechi ya AS Vita ataanza na viungo wanne kama katika mechi iliyopita dhidi ya JS Saoura ambao, walicheza nyumbani na kupata ushindi wa mabao 3-0.

Katika mazoezi ya mwisho ya kimbinu zaidi ambayo walifanya kule Dar es Salaam uwanjani Boko Veterans, Aussems alianza na viungo wawili wakabaji ambao ni James Kotei na Jonas Mkude na viungo wengine wawili washambuliaji. Katika eneo la kiungo mshambuliaji Clatous Chama ameonekana kuingia moja kwa moja akicheza kama winga wa kulia huko viungo watatu, Haruna Niyonzima, Hassan Dilunga na Mzamiru Yassin walikuwa wakicheza kwa kupishana katika kikosi cha kwanza.

Niyonzima, Dilunga na Mzamiru walionekana kumvuruga Aussems kwani, kila aliyekuwa akipewa nafasi ya kufanya mazoezi na kikosi cha kwanza, anafanya vizuri na kesho yoyote anaweza kuanza katika kikosi cha kwanza.

Akizungumza na Mwanaspoti, Aussems alisema mazoezi ya mbinu waliyofanya Dar es Salaam ndio watayatumia katika mechi ya AS Vita kwani, hawatakuwa na muda mwingine wa kufanya mazoezi hayo.

“Siwezi kusema mchezaji gani ataanza katika kikosi cha kwanza, lakini wote ambao nitasafiri nao wana uwezo wa kupata nafasi na ili kupambana na kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” alisema.

Kulingana na mazoezi ya mwisho kikosi cha Simba kitaanza na kipa Aishi Manula, Nicholas Gyan, Mohammed Hessein ‘Tshabalala’, Juuko Murushid, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Clatous Chama, James Kotei, Okwi, Kagere na Niyonzima, Dilunga au Mzamiru mmoja kati ya hawa anaweza akaanza.

MSIKIE MSOLLA

Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Dk Mshindo Msolla akizungumzia kuhusu viungo wa kikosi hicho alisema: “Niyonzima kwa sasa ametambua nini anatakiwa kufanya ndiyo maana kiwango chake kimepanda tofauti na siku za nyuma, ila sio mchezaji wa kutegemea kubadilisha matokeo.”

Imeandikwa na Khatimu

Naheka, Kinshasa, Thobias Sebastian na Mwanahiba

Richard, Dar es Salaam.