Simba yafichua siri za Morrison

HUKO mitaani, mashabiki wa Simba wamekuwa wakiwaambia wenzao wa Yanga, kwamba wajiandae kupata maumivu wakati mabosi wao watakavyowavuta kikosini kina Bernard Morrison na nahodha wake, Papy Kabamba Tshishimbi.

Licha ya kuelezwa Morrison ameshasaini Yanga, huku Tshishimbi kila kitu kikielekea pazuri, Jangwani, lakini presha wanazopata kwa watani wao zinawakosesha raha, lakini mabosi wa Msimbazi wameanika siri ambayo inaweza kuwatuliza Wanayanga kwa ujumla.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa amepuuzia taarifa kwamba eti Morrison alishapewa kabisa kishika uchumba ili atue Msimbazi na kwa sasa nguvu imeelezwa kwa Tshishimbi akidai hakuna kitu kama hicho na wala hawajawahi kuwafikiria nyota hao wa Yanga.

Senzo, alisema licha ya kusoma kila uchao taarifa za nyota hao wa Yanga kuhusishwa na klabu yake, lakini kama Mtendaji Mkuu hajawahi kuletewa mezani majina ya wachezaji hao wala kuwa na mapendekezo ya kocha wao, Sven Vandenbroeck.

Mtendaji huyo alisisitiza kwa kipindi hiki, hawadili na mambo ya usajili wanachokifanya ni kuangalia ni namna gani kwenye timu yao wasikumbwe na janga la ugonjwa wa virusi vya Corona kwani ni janga la dunia.

“Binafsi sina taarifa juu ya tetesi hizo za wachezaji kutakiwa kusajiliwa kwetu na huwa sipendelei sana kufanyia kazi tetesi. Kama jambo lipo basi linakuwa limejadiliwa na kocha anakuwa ameleta mapendekezo ya wachezaji anaowataka,” alisema Senzo na kuongeza;

“Kwasasa tunaangalia ni namna gani ya kupambana na Corona ili isije ikaathiri kwenye timu yetu hasa kipindi cha kuanza mechi za ligi, usajili si jambo kubwa kama lilivyo suala la vita dhidi ya Corona.”

Senzo alisema mambo mengi yamesimama kwasasa kupisha janga la Corona hivyo hata wakifanya usajili na bado kukawa na mlipuko mkubwa wa maambukizi itakuwa haina maana kwao.

“Ndiyo maana hata kwenye kikao chetu cha jana (juzi Jumanne) tuliwapa programu nyingine wachezaji wetu ili waendelee kuzifanya majumbani maana bado mapambano ya Corona ni makubwa hatuwezi kuwakusanya kipindi hiki.

“Programu hiyo ya kufanya mazoezi binafsi huko waliko itaendelea hadi hapo ambapo TFF (Shirikisho la Soka nchini) litakapotangaza tarehe ya kuanza kwa ligi, hivyo hatuwezi kuingiza timu kwasasa bila kujua hilo,” alisema