Simba yaifunga mdomo Yanga Taifa ikiilaza bao 1-0

Dar es Salaam. Timu ya Simba imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya watani zao Yanga kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara mechi iliyopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo Jumamosi.

Ushindi huo wa Simba, umewafanya kusogea nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu wakifisha alama 39.

Bao pekee la ushindi kwa Simba lilifungwa na Meddie Kagere dakika ya 71 kipindi cha pili ikiwa ndio bao lake la kwanza kwenye mechi ya watani wa jadi.

Hata hivyo Yanga ndio wanaoongoza Ligi wakiwa na alama 58 wakiwa wamecheza raundi ya 22 huku Simba wakiwa wamecheza 16.

Mchezo wa Yanga na Simba ulionekana kuwa  wa ubabe, kuliko kutumia mbinu za ufundi katika dakika 45 za kwanza zimemalizika kwa suluhu.

Katika mchezo huo Simba walikuwa wakitumia zaidi uoande wa kulia uliokuwa ukichezwa na beki Zana Coulibaly, ambaye alionekana kuwa na uharaka katika kupeleka mashambulizi na kupiga krosi.

Kwa upande wa Yanga wao walionekana kukaba zaidi kutokana na kutokuwa na mipango dhabiti ya kushambulia tofauti na kwa upande wa Simba.

Dakika 6 Simba walipata kona baada ya Gadiel Michael kuutoa mpira, hata hivyo kona hiyo iliyopigwa na Emmanuel Okwi haikuwa na faida.

Yanga waliamka na kuamua kutumia mipira mirefu katika kupeleka mashambulizi, staili hiyo ilionekana kwao bora kutokana na kushindwa kuweka mipira chini.

Dakika 7 Paul Godfrey alianzishiwa pasi fupi na Ibrahim Ajib, alipiga shuti kali na kupaa pembezoni mwa mwamba wa juu.

Simba walizidi kushambulia zaidi lakini walikuwa hawawezi kupita katikati ya mabeki Andrew Vicent na Kelvin Yondani.

Dakika 17 Simba walipata kona nyingine lakini hata hivyo umakini wa Simba ulikuwa mdogo na kushindwa kufanya vizuri katika kona hizo mbili walizopata.

Beki Paul Godfrey dakika 23 alipanda kwa spidi na mpira lakini beki wa Simba,Mohammed Hussein alimfanyia madhambi na kaudhibiwa kwa kupewa kadi ya njano.

Faulo fupi iliyopigwa na Ibrahim Ajib, ilitaka kuzaa bao hata hivyo umakini wa Andrew Vicent ulikuwa mdogo na kushindwa kuipa bao Yanga.

Yanga walionekana kufunguka baada ya kucheza takribani dakika 24 bila kushambulia, dakika 25 walikosa goli baada ya Ajib kumpigia Makambo pasi mpenyezo na kuunganisha lakini hata hivyo ulipaa juu kidogo ya goli.

Ndani ya dakika 33 za mchezo huu, Simba walionekana kuwa watulivu zaidi kuliko Yanga kwenye kuhakikisha wanapeleka mashambulizi.