Simba yaipa presha Azam

Mwanza. Simba imejiweka katika mazingira mazuri ya kushika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya jana kuichapa Alliance mabao 2-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Tangu Novemba, mwaka jana Simba ilikuwa ikishika nafasi ya nne au tatu ambayo ilidumu nayo kwa muda mrefu na kuziacha Yanga na Azam zikipokezana kushika usukani wa Ligi Kuu.

Endapo Simba itashinda mchezo wa kesho dhidi ya KMC itapanda hadi nafasi ya pili na kuishusha Azam ambayo imedumu kwenye nafasi hiyo muda mrefu. Simba ikiifunga KMC itafikisha pointi 66 sawa na Azam lakini itanufaika kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Pia Simba itakuwa na fursa nzuri ya kubaki katika nafasi hiyo kama itashinda mechi yake dhidi ya Biashara United Aprili 27 na mechi nyingine zitakazofuata.

Endapo Simba itapanda nafasi ya pili itaongeza presha kwa Yanga ambao wanapambana kuhakikisha wanatwaa ubingwa msimu huu. Yanga inaongoza ligi kwa pointi 74. Endapo Simba itashinda mechi 13 zilizobaki itafikisha pointi 102 na kuwa mabingwa wakati Yanga ikishinda michezo sita itafikisha pointi 92.

Mchezo ulivyokuwa

Kipindi cha kwanza kilianza kwa kasi huku Simba ikitawala mchezo kwa kutengeneza nafasi kadhaa ikiwemo ya dakika ya sita ambayo Haruna Niyonzima alikosa bao akiwa ndani ya 18.

Simba ililisakama lango la Alliance na juhudi zake zilizaa bao dakika ya 20 lililofungwa na Niyonzima kwa kiki ya karibu akiunganisha krosi ya Mzamiru Yassin.

Alliance ilipambana lakini ilizidiwa mbinu na Simba na dakika ya 27 Chinedu Michael alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumchezea rafu Mzamiru, pia John Bocco alipata adhabu hiyo kwa kumtolea maneno mwamuzi Ahmada Simba wa Kagera. Kocha wa Simba Patrick Ausems alifanya mabadiliko kwa kumtoa Hassani Dilunga, Adam Salamba na nafasi zao kujazwa na Clatous Chama na Emmanuel Okwi. Dakika ya 62 Okwi aliipatia Simba bao la pili baada ya kuwapiga chenga mabeki watatu wa Alliance na kutumbukiza mpira wavuni.

Alliance: John Mwenda,Godlove Mdumule, Siraji Juma, Joseph James, Godfrey Lusekeye, Juma Nyangi, Mcharo John, Shabani Willium, Michael Chinedu, Balama Mapinduzi na Dickson Ambundo.

Simba:Aishi Manula, Nicholas Gyan,Asante Kwasi, Juuko Murshid, Yusuph Mlipili, Said Ndemla, Muzamiru Yassin, Hassan Dilunga, Adam Salamba,John Bocco na Haruna Niyonzima.