Simba yaishusha Azam Ligi Kuu

Mwanza. Mabao ya Emmanuel Okwi na John Bocco yalitosha kuipandisha Simba hadi nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara huku ikifikisha penalti nne katika mechi tano.

Simba ilipata penalti dhidi ya Mbao, Coastal Union na jana ilipata mbili dhidi ya KMC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza. Simba ilishinda mabao 2-1.

Okwi amefunga bao la tatu katika mechi ya tatu mfululizo akiwa ugenini baada ya kuzifunga Kagera Sugar, Alliance na KMC.

Wakati mchezaji huyo wa kimataifa wa Uganda akifikisha mabao 10, Bocco ameweka wavuni mabao 12 katika mechi za Ligi Kuu msimu huu.

Simba imepanda hadi nafasi ya pili baada ya kufikisha pointi 66 na kuishusha Azam iliyokaa katika nafasi hiyo kwa muda mrefu. Pia Azam ina pointi 66 lakini Simba ina uwiano mzuri wa idadi ya mabao.

Simba imefunga mabao 55, imefungwa 11 wakati Azam imefunga mabao 49 na kuruhusu 19 hivyo kuwa na tofauti ya mabao 44 na 30. KMC imebaki nafasi ya saba katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 42. KMC jana ilicheza kwa kiwango bora mchezo huo licha ya kufungwa.

Mchezo ulivyokuwa

Simba ilianza mchezo huo kwa kasi na ilitumia dakika 10 kupata kona iliyopigwa na Clatous Chama, ambayo hata hivyo haikuzaa matunda.

Dakika ya 14 Bocco alikosa bao baada ya kushindwa kumalizia pasi safi iliyopigwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere.

Simba iliendelea kulisakama lango la KMC na kupata bao kattika dakika ya 22 lililofungwa na Okwi kwa kiki akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na James Kotei.

Faulo hiyo ilitokana na Yusufu Ndikumana kumfanyia madhambi Bocco. KMC ilizinduka na kupata bao katika dakika ya 57 lililofungwa na Hassani Kabunda aliyemzidi mbio beki wa Simba, Zana Coulibally na kuutumbukiza mpira nyavuni.

Simba ingepata bao jingine kama Kagere asingekosa penalti ya dakika ya 61 baada ya kupiga kiki iliyodakwa na kipa wa KMC Jonathan Nahimana.

Simba ilipata bao la pili katika dakika ya 81 kwa penalti kupitia kwa Bocco. Hata hivyo, penalti iliibua mzozo kwa wachezaji kumalalamikia mwamuzi Abdallah Kambuzi wakidai haikuwa halali.

KMC: Jonathan Nahimana, Aron Kalambo, Ally Ramadhani, Ismail Gambo, Yusuf Ndikumana, Masoudy Abdallah, Abdul Hilary, George Sangijo, Omary Ramadhani, Ally Mjengi na Hassan Kabunda.

Simba: Aishi Manula, Zana Coulibally, Mohammed Hussein, Yusuf Mlipili, Erasto Nyoni, James Kotei, Clatous Chama, Jonas Mkude, John Bocco, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi.