Simba yaizidi kete Nkana

Muktasari:

Simba inaivaa Nkana ikifahamu ushindi dhidi ya wapinzani wao katika mechi mbili za nyumbani na ugenini utawafanya wafuzu hatua ya makundi kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kuanza vyema mechi ya hatua ya awali kwa kuing’oa Mbabane Swallows ya Swaziland

Dar es Salaam.Ushindi wa Simba dhidi ya Nkana Red Devils katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huenda ukachagizwa na sababu kubwa nne zitakazowapa chachu wawakilishi hao wa Tanzania Bara.

Kiu ya kufuzu hatua ya makundi, hamu ya kumaliza unyonge dhidi ya timu za Zambia na uimara wa kikosi cha Simba msimu huu pia udhaifu wa safu ya ulinzi na ushambuliaji unaoendana na rekodi isiyoridhisha ya Nkana katika mashindano ya kimataifa siku za hivi karibuni, vinatoa ishara njema kwa Wekundu wa Msimbazi kuwaondosha Wazambia hao.

Simba inaivaa Nkana ikifahamu ushindi dhidi ya wapinzani wao katika mechi mbili za nyumbani na ugenini utawafanya wafuzu hatua ya makundi kwenye mashindano hayo.

Tangu ilipofuzu hatua hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003 baada ya kukitupa nje kigogo Zamalek, Simba haikuweza tena kuifikia ingawa watani wao wa jadi Yanga walifanya hivyo kwenye Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2016 na mwaka huu.

Hasira za Simba bila shaka ndizo zilizochangia timu hiyo kufanya maandalizi kabambe ikiwemo kutenga bajeti ya Sh6 bilioni msimu ambao itajumuisha masuala ya usajili na huduma za timu ili waweze kuwa katika daraja la kuhimili vishindo vya mashindano hayo.

Hata hivyo kiu ya Simba kuiondosha Nkana kuingia hatua ya makundi inachochewa na hasira na tamaa ya kulipa kisasi kwa timu za Zambia hasa wapinzani wao hao ambao wamekuwa wakiwaonea wawakilishi hao wa Tanzania Bara mara kwa mara kila wanapokutana.

Hii itakuwa ni mara ya tatu kwa Nkana kupangwa na Simba kwenye hatua mbalimbali za mashindano ya kimataifa ambapo kabla ya hapo walipangwa mwaka 1994 na 2002.

Katika Kombe la Washindi mwaka 1994 ambapo Simba ilikuwa chini ya ufadhili wa Azim Dewji, Nkana iliwatoa wawakilishi hao wa Tanzania kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3 kwenye robo fainali ya Kombe la Washindi Afrika.

Nkana ilianza kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 katika mechi ya kwanza Zambia na walipokuja nchini kwenye mechi ya marudiano, Simba ilishinda 2-0. Pia mwaka 2002, Nkana iliitupa tena nje Simba kwa ushindi wa jumla kama ule wa mwaka 1994 wa mabao 4-3.

Katika mechi ya kwanza iliyochezwa Zambia, Simba ilichapwa mabao 4-0 na ziliporudiana Nkana ilifungwa 3-0. Tangu mwaka 1974, Simba imeshinda mara tatu kati ya michezo mitano iliyocheza dhidi ya timu za Zambia katika mashindano ya Afrika.

Mwaka 1974, Simba ilitoa Green Buffaloes kwa jumla ya mabao 3-1 katika Kombe la Mabingwa Afrika. Awali, ilishinda 2-1 kabla ya kuilaza bao 1-0.

Mwaka 1976, Buffaloes iliing’oa Simba kwa jumla ya mabao 4-2, mchezo wa kwanza Simba ilichapwa 3-2 na ziliporudiana ilifungwa bao 1-0.

Simba ilirudi Zambia mwaka 1995 na kufanikiwa kuitoa Power Dynamos kwa penalti 3-4 baada ya mechi mbili za nyumbani na ugenini kutoka sare ya bao 1-1 hivyo matokeo ya jumla kuwa 2-2 kabla ya kutumika mikwaju ya penalti.

Mwaka 2004, Simba ilitolewa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Zanaco baada ya kuchapwa jumla ya mabao 3-2. Mchezo wa kwanza Simba ilishinda 1-0, lakini mechi ya marudiano Zanaco ilishinda 3-1 na kusonga mbele.

Lakini pamoja na hilo, Simba iliyo na kikosi bora kwa sasa kilichoing’oa Mbabane Swallows iliyocheza hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika mara mbili mfululizo mwaka 2017 na 2018, inakutana na Nkana ambayo ina upungufu kadhaa unaoweza kuwabeba wawakilishi hao wa Tanzania Bara.

Udhaifu wa Nkana ni kuwa na safu ya ulinzi inayoruhusu mabao iwe inacheza ugenini au nyumbani kwenye mashindano hayo ya kimataifa.

Katika mechi 10 za mwisho za mashindano ya kimataifa, nyavu za Nkana zimetikiswa mara 13 sawa na idadi ya mabao waliyofunga huku mechi tatu tu ndiyo wakicheza bila kuruhusu mabao.

Hivyo ni tofauti na Simba ambayo kwenye mechi zake sita za mwisho za kimataifa, imefunga mabao 15 huku ikiruhusu nyavu zake kuguswa mara tatu tu.

Hofu kubwa ya timu za Tanzania ni pale zinapokwenda ugenini lakini bahati njema kwa Simba Nkana imekuwa ikiruhusu nyavu zake kutikiswa pindi ikiwa nyumbani, katika mechi 10 za mwisho za kimataifa ilizocheza nyumbani, imeruhusu mabao tisa huku yenyewe ikifunga mabao 16, imeibuka na ushindi mara tano na kutoka sare tano.

Ugenini, Nkana huwa wanyonge zaidi kwani katika michezo 10 ya mwisho ya kimataifa ikiwa ugenini, imepoteza mechi saba, imeshinda mbili na kutoka sare mmoja, imefunga mabao nane na nyavu zake kutikiswa mara 24 na hakuna hata mechi moja ambayo ilimaliza bila kuruhusu bao.

Nyota ambao Simba inapaswa kuwachunga zaidi ni Walter Bwalya, Kelvin Mubanga na Chisamba Lungu ambao ni tegemeo.