Simba yajiweka pabaya ligi kuu

Dar es Salaam. Mechi nane za viporo huenda zikavuruga hesabu za Simba kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa itashindwa kuchanga vyema karata zake na kuibuka na ushindi kwenye michezo hiyo.

Wakati Ligi Kuu ikiwa imefika raundi ya 22, Simba imecheza mechi 14 tu zinazoiweka nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi na pointi 33 nyuma ya Yanga inayoongoza kwa pointi 53 na Azam FC pointi 41.

Mechi hizo nane za viporo ambazo Simba inazo mkononi ni dhidi ya Mwadui, Biashara United, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Azam FC, Lipuli, Coastal Union na Prisons.

Ushindi wa Simba katika mechi hizo nane utaifanya ifikishe pointi 57 ambazo zitakuwa tano pungufu ya Yanga inayoongoza ligi ikiwa nayo itashinda mechi tatu za viporo zitakazoifanya iwe na idadi sawa na timu nyingine kwenye ligi.

Nafasi ya Simba kutetea ubingwa ambao utaifanya ipate nafasi ya kuwakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, ipo mikononi mwa mechi hizo nane ambazo zinaweza kugeuka shubiri kwao ikiwa watashindwa kufanya vizuri.

Uwezekano wa Simba kutwaa ubingwa huo ambao ndio njia pekee iliyobaki kwao kupata tiketi ya kucheza mechi za kimataifa msimu ujao, huenda ukaathiriwa na viporo hivyo kutokana na sababu mbalimbali.

Kwanza Simba italazimika kucheza mechi za kiporo ikiwa na presha kubwa kutokana na kasi ya wapinzani wao Yanga katika Ligi Kuu msimu huu ambapo hawajapoteza mchezo kati ya 19 waliyocheza hadi sasa huku wakitoka sare mechi mbili tu.

Presha ya Yanga haisababishwi tu na ushindi ambao wanaupata bali pia pengo la pointi lililopo baina yao na Simba ambalo hadi sasa ni pointi 20.

Lakini pia Simba itacheza mechi hizo za viporo huku ikiwa na uchovu utokanao na ushiriki wake kwenye mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambazo zimepangwa kuchezwa ndani ya kipindi kifupi jambo litakalowafanya wasipate muda wa kutosha kupumzika.

Ukiondoa sababu hizo, kingine ambacho huenda kikaigharimu Simba ni hofu itokanayo na rekodi yao isiyovutia ya kufanya vibaya kwenye mechi za viporo ambazo zimekuwa zikiwasumbua mara kwa mara tofauti na Yanga.

Mfano wa hilo unajidhihirisha katika msimu wa 2015/2016 ambao Simba ilikuwa na viporo vinne dhidi ya Majimaji, Toto Africans, Azam na Mwadui.

Katika mechi hizo, ilitoka sare mbili dhidi ya Majimaji na Azam na ilipoteza viporo viwili nyumbani ilipocheza na Mwadui na Toto Africans kwa kipigo cha bao 1-0 katika kila mechi.

Lakini Yanga kwa misimu miwili tofauti ilithibitisha hawatishwi na viporo ambapo msimu wa 2014/2015 ilivuna pointi tisa katika mechi tatu dhidi ya JKT Ruvu, Coastal Union na Stand United.

Katika msimu wa 2016/2017, Yanga ilikuwa na viporo vinne mkononi dhidi ya Simba ambapo ilishinda vyote dhidi ya JKT Ruvu, Ruvu Shooting na Toto Africans huku ikitwaa ubingwa wa Ligi Kuu.

Akizungumza jana, mkurugenzi wa zamani wa mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Saad Kawemba alitaja mambo matatu muhimu ya kuzingatia katika upangaji wa ratiba hiyo ambayo ni kutafuta watalamu wa teknolojia ya mawasiliano (IT) ama kuwapeleka watu wakasomee na kama itashindakana alishauri zinunuliwe programu za kuwasaidia kufanya kazi hiyo.

“Jambo la pili kunapokuwepo mashindano ya kimataifa ni vyema ligi ikasimama ili kuipa thamani yake, pia hilo litasaidia kupunguza pengo la kupishana mechi nyingi, mfano wapo waliocheza 20 huku wengine 14 kitu ambacho hakileti afya ya soka nchini.

“Ifikie hatua ya kuacha kupanga ratiba kwa uzoefu, mambo kwa sasa yanaenda kisasa zaidi lasivyo hivyo vitu visipozingatiwa vitahatarisha ushindani wa soka na kitakachofuata kwa wale ambao wana mechi nyingi ni kucheza kwa mfululizo kitu ambacho siyo taaluma ya kazi hiyo,”alisema Kawemba.

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Boniface Wambura alisema atatolea ufafanuzi wa suala hilo leo.

“Leo (jana) nilikuwa nizungumze na wanahabari kuwapa ufafanuzi juu ya hilo, lakini kwa bahati mbaya tumepatwa na msiba,” alisema Wambura.

Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa aliliambia gazeti hili kuwa mechi za viporo ni mtego wa hatari kwa Simba.

“Ninachokiamini mimi hakuna kitu kibaya kama mechi za viporo kwa sababu unakutana na timu ambayo inakuwa imepata muda wa kutosha kujiandaa,” alisema Pawasa.