Simba yaonyesha jeuri mpya

SIMBA Jeuri bwana! Wamepiga hesabu zao na kujiridhisha bado wanaweza kuwa na pumzi ya kutosha kwa miezi kadhaa wala corona haiwezi kuathiri akaunti za wachezaji wao.

Mmoja wa vigogo wa muda mrefu ndani ya Simba, ambaye pia ni mjumbe mzito kwenye bodi ya klabu ya Simba, Mulamu Ng’ambi ameliambia Mwanaspoti wamejipanga na tathmini yao imewaonyesha wanaweza kujiendesha bila mapato ya milangoni hivyo hata ikiendelea kusimama hawawezi kuathirika kiasi cha kushindwa kulipa mishahara ya wachezaji.

Mulamu ambaye ni mtu wa karibu wa Bilionea, Mohammed Dewji Mo ambaye ndiye mwezeshaji na mwekezaji wa Simba alisema wamegundua viingilio vya mechi zao ni sehemu ndogo tu ya kuongeza kipato ndani ya klabu hiyo.

Alisema kusimama kwa ligi hakuwezi kuathiri mwenendo wa klabu hiyo ikiwemo malipo ya mishahara kwa wachezaji kwani hawawezi kuwakata kila mmoja atapata stahiki zake kwa mujibu wa makuliano.

Ingawa hakuweka wazi lakini Mwanaspoti wiki iliyopita, liliambiwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa kila mwezi wanalipa Dola 100,000 (sawa na zaidi ya Sh230 milioni) kwa mwezi ambazo asilimia kubwa zinatoka kwa Mo na wadhamini wengine wa Simba.

“Simba ina vyanzo vingi vya pesa, hivyo kusimama kwa ligi hakuwezi kuathiri mwenendo wa timu kwani kulipa mishahara kuko pale pale,” alisema Mulamu na kuongeza kwenye usajili wataziba mapengo muhimu ambayo yatahitajika kutokana na mapendekezo ya benchi la ufundi chini ya Kocha Sven Ludwig Vanderbroeck.

“Simba iko vizuri kwa sehemu kubwa, kocha analeta mapendekezo ya wachezaji anaowahitaji ila hawatakuwa wengi,” alisisitiza kiongozi huyo.