Simba yarejea na tabasamu, kufanya mazoezi Boko Veterans leo

Muktasari:

  • Kikosi cha Simba kimerejea jijini Dar es Salaam na leo Jumatano kitafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Boko Veterans kujiandaa na mchezo mwingine wa Ligi Kuu Bara.

Simba inatarajiwa kucheza na Azam FC  siku ya Ijumaa mchezo utakaopigwa Uwanja wa Taifa ambapo wenyeji watakuwa vijana hao wa Chamazi.

 Jana Jumanne, Simba iliibuka na ushindi mnono kwa kuichapa African Lyon mabao 3-0 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid leo Jumanne.

Mabao ya Simba yalifungwa na John Bocco (2) huku Peter Salamba akitupia wavuni bao moja.

Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha alama 42 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikisalia nafasi ya tatu.

Katika mchezo huo Simba waliwaanzisha Aishi Manula, Asante Kwasi, Nicholas Gyan, Paul Bukaba, Pascal Wawa, Mzamiru Yassin, Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Adam Salamba, john Bocco na Rashid Juma.

Kwenye  kikosi hiko ni nyota watatu tu ambao walioanza katika mchezo wa Ligi Kuu uliopita waliocheza dhidi ya Yanga, ambao ni Aish Manula, Pascal Wawa na John Bocco.

Katika kipindi cha kwanza timu zote zilikuwa zikicheza kwa kukamiana huku wakitumia spidi kupeleka mashambulizi yao kwa kuvizia langoni mwa mwenzake.

Simba walionekana kutaka goli la kuongoza lakini hata hivyo mipango yao iliokena kuwa hafifu kwani walishindwa kuipasua safu ya ulinzi ya African Lyon.