Simba yasafisha nyota ya Uturuki kwa Arusha United

Arusha. Timu ya Simba sc kwa mara ya kwanza imeambulia ushindi wa bao 2-1 katika mchezo mitatu ya kirafiki waliyocheza baada ya kutoka nchini Uturuki wakiwa chini ya kocha Patrick Aussems.

Mchezo huo ulianza kwa kasi kwa upande wa Simba na ikachukua dakika 7 Emmanuel Okwi kuiandikia timu yake bao la kuongoza lakini Arusha United walisawazisha dakika ya 17 lililofungwa na Ally Kabunda kabla ya Okwi kurudi tena wavuni dakika ya 29.

Arush United alionekana kurudi mchezoni baada ya mlezi wa timu hiyo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kutangaza dau kwa kila bao sh 500,000 katika kipindi cha kwanza huku kipindi cha pili dau likiongezeka mara mbili kwa kila bao.

Katika mchezo huo mlinda mlango wa Arusha United, Rahim Shekhe kuonekana kinara wa mchezo baada ya kuokoa hatari nyingi zilizokuwa zinapelekwa langobi mwao ikiongozwa na Okwi pamoja na Meddie Kagere.

Arusha United wanatarajia kucheza michezo mingi ya kirafiki katika kuimalisha kikosi chake huku Simba wakisafiri kuelekea mwanza kwa ajili ya mchezo wa ngao ya jamii dhidi ya Mtibwa mwishoni mwa wiki katika Uwanja wa CCM Kirumba.