Simba yashusha Mbrazili wa kurithi mikoba ya Juuko

Muktasari:

  • Usajili wa mchezaji huyu ni dhahiri Simba wameamua kuachana na beki Juuko Murshid ambaye yupo katika fainali za Afcon akiwa na kikosi cha Uganda.

Dar es Salaam. Mabosi wa Simba wameendelea na tambo za usajili baada ya kukamilisha usajili Mbrazili Gerson Fraga Vieira kwa mkataba wa miaka miwili.

Uongozi wa Simba kupitia kwa muwekezaji wao tajiri Mohammed Dewji aliwahi kukaririwa akisema watafanya usajili mkubwa wa kushindana na TP Mazembe pamoja na Zamalek.

Leo mchana kiraka huyo alitambulishwa akiwa pamoja na mmoja wa viongozi wa bodi Simba, Zacharia Hanspope.

Usajili wa mchezaji huyu ni dhahiri Simba wameamua kuachana na beki Juuko Murshid ambaye yupo katika fainali za Afcon akiwa na kikosi cha Uganda.

Gerson mwenye umri wa miaka 26 alianza kucheza soka akiwa kijana katika akademi ya Gremio (2000 hadi 2013) nchini Brazil.

Aliichezea timu ya Vijana Brazil chini ya miaka 15 mwaka 2007 na walifanikiwa kuchukua ubingwa wa Mediterranean International Cup.

Pia aliichezea timu ya Brazil chini ya miaka 17 mwaka 2009 mpaka kombe la Dunia akiwa kapteni katika timu hiyo.

Katika ngazi ya klabu  amecheza katika timu ya Gremio Ligi ya Brazil, Seria A (2013-2015), 2016-2017 ameichezea Mumbai City inayoshiriki Indian Super League, 2017-2018 Aliichezea Renota Yamagushi, Japan na  2018-2019 Aliichezea India Atletico de Kolkata ATK ambao ndio mabingwa wa Ligi ya India.