Simba yatangaza Bajeti Sh6 bilioni, usajili dirisha dogo Sh76.8 milioni

Muktasari:

Mo Halisi Sabuni ya Unga pamoja na Mo Extra wametangaza udhamini wao ni jumla ya Sh 400 milioni kwa mwaka mmoja.

Dar es Salaam. Simba imetangaza bajeti ya Sh6.1 bilioni kwa msimu huu 2019/2020 katika kuhakikisha klabu hiyo itatetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kurudi katika Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

Bajeti hiyo imetajwa kwenye mkutano mkuu wa klabu ya Simba unaoendelea jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere.

Katika bajeti hiyo, klabu ya Simba imetenga Sh76.8 Milioni za usajili wa dirisha dogo utakaoanza hivi karibuni.

Mbali na usajili wa dirisha dogo, klabu ya Simba itatumia Sh 4.16 Bilioni kwa ajili ya mishahara ya wachezaji na Sh 408 kwa ajili ya bonusi.

Katika bajeti hivyo, vyanzo vya mapato vitaiingizia klabu ya Simba Sh 5.814 Bilioni ambayo ni pungufu ya Sh373 milioni katika mapato ya klabu.

MO Halisi sabuni yaweka ubaoni Sh400 milioni

Katika hatua nyingine bidhaa ya Mo Halisi Sabuni ya Unga ni miongoni mwa mdhamini mwingine ndani ya Simba baada ya kuwepo wadhamini wengine.

SportPesa ndio wadhamini wakuu wa Simba, Mo Extra, Azam Tv na Uhlsport ambao walitangazwa rasmi siku za nyuma.

Katika jezi za wachezaji wa Simba, mgongoni yameandikwa maneno ya udhamini wa Mo Halisi Sabùni ya Unga

Mo Halisi Sabuni ya Unga ambayo ni bidhaa iliyo chini ya Kampuni ya Mohemed Dewji ambaye ni Mwekezaji na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba inakuwa bidhaa ya pili baada ya Mo Extra iliyotoa Sh250 milioni.

Mhasibu Mwandamizi wa Simba, Suleiman Kahumbu amesema Mo Halisi Sabuni ya Unga pamoja na Mo Extra udhamini wao ni jumla ya Sh 400 milioni kwa mwaka mmoja.

Kahumbu amesema bado kuna wadhamini wengine ambao hakuweza kuwaweka wazi kwenye mkutano mkuu wa mwaka unaondelea kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.