Sindano tano kwa Katibu Mkuu Yanga

Muktasari:

  • Kuteuliwa kwa Ruhago kuna maana Katibu Mkuu anakabiliwa na kazi ngumu ya kupambana nayo na Mwanaspoti linakuletea mambo matano ambayo katibu huyo anapaswa kupambana nayo.

YANGA imeanza maisha mapya ikiwa na Katibu Mkuu Mpya, Dk David Ruhago ambaye mpaka leo ikikatika atakuwa anamaliza siku ya nne tangu atangazwe rasmi, lakini ujio wake ndani ya nafasi hiyo atakabiliwa na mambo matano mazito kuthibitisha ubora wake.

Ruhago, ambaye ujio wake ndani ya Yanga ulianzia katika kamati maalumu ya kukusanya fedha kwa ajili ya usajili wa msimu huu, Novemba 11 wiki hii alitangazwa kuchukua nafasi ya Katibu Mkuu wa klabu hiyo, mchakato uliodumu kwa siku 189 tangu uongozi mpya chini ya Mwenyekiti Dk Mshindo Msolla uingie madarakani Mei 6, 2019.

Kuteuliwa kwa Ruhago kuna maana Katibu Mkuu anakabiliwa na kazi ngumu ya kupambana nayo na Mwanaspoti linakuletea mambo matano ambayo katibu huyo anapaswa kupambana nayo.

Kurudisha nguvu ya sekretarieti

Jukumu la kwanza ambalo Ruhago atakumbana nalo litakuwa ni kurudisha nidhamu ya kazi katika sekretarieti itakayokuwa chini yake katika muda wa uongozi wake.

Mpaka sasa Yanga imepanua Sekretarieti hiyo ikiwa na nafasi mpya tatu ambazo ni Kurugenzi ya Mashindano, Ofisa Mhasishaji Mkuu, Kurugenzi ya Ufundi ambazo zitaungana na ajira nyingine za Afisa Habari, Mkurugenzi wa Fedha, Ofisa Masoko na Ofisi ya Mwanasheria wa Klabu.

Kimsingi Ruhago atahusika katika mapungufu yote katika muundo huo kuhakikisha kwamba watendaji wote waliochini yake wanaleta mafanikio katika uongozi wake na kufuta mapungufu yote yaliyojitokeza kwa watangulizi wake.

Mipango ya maendeleo

Eneo la pili ambalo Ruhago atatakiwa kukabiliana nalo ni kuhakikisha ofisi yake inakuwa na tija katika mipango ya maendeleo hasa kuwa na msukomo katika kubadilisha mfumo wa uendeshwaji pamoja na kuongeza kipato kwa klabu hiyo kupitia udhamini na hata kuuza wachezaji.

Kubwani kuhakikisha pale alipoishia mtangulizi wake, Charles Boniface Mkwasa, juu ya ishu ya Uwanja wa Kaunda uliopo Jangwani. Hatua kubwa ambayo katibu wa mwisho Charles Mkwasa aliiacha ni juu ya kujaza kifusi katika eneo la uwanja wa Kaunda na kufanikiwa kukimbiza hali ya kujaa maji na sasa zigo hilo litatua kwa Ruhago katika kuendeleza eneo hilo, pia Yanga kuwa na uwanja wake wa mazoezi.

Pia Dk. Ruhago tayari anakuta biashara ya jezi na vifaa vingine ikiwa imeshaanza ndani ya klabu hiyo na sasa ustawi wa dili hilo lililopo chini ya GSM sasa litakuwa chini ya usimamizi wake.

Kukubalika kwa wanachama

Hatua mbaya kwa Ruhago ni pia inaelezwa uteuzi wake awali ulikutana na kasheshe la kupingwa na baadhi ya wanachama kabla ya mambo kuwekwa sawa na sasa kutangazwa kwake kisha kuanza kazi atatakiwa kuwa kiungo mzuri kati ya wanachama hao pamoja na uongozi kwa kufanya mambo makubwa na kuwanyamazisha waliokuwa wanampinga.

Endapo Ruhago atashindwa kukata kiu ya wanachama wa klabu hiyo kwa kufanya mambo ya maendeleo, hatua hiyo itazidi kumwongezea presha katika nafasi yake ambapo wale waliompinga huenda wakapata nafasi ya kumshambulia zaidi sambamba na uongozi mzima.

Pambano la Watani

Linaweza kuwa jambo dogo, lakini kwa maisha ya klabu za Simba na Yanga ni kitu kikubwa Dk. Ruhago atakabiliwa na changamoto ya mechi ya watani ambayo imepangwa kufanyika Januari 4 mwakani, ikiwa ni wiki chache baada ya Ligi Kuu kusimama kwa muda kupisha michuano kadhaa ya kimataifa na ile ya Mapinduzi.

Bahati mbaya, anachukua cheo hicho wakati Yanga ikiwa haijaonja ushindi dhidi ya Simba tangu Februari 2016 waliposhinda mara ya mwisho mabao 2-0 yaliyowekwa kimiani na Donald Ngoma na Amissi Tambwe ambao kwa sasa hawapo kikosini.

Katika mechi sita zilizopiota tangu waliposhinda mara ya mwisho katika Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba, Yanga imepoteza mechi tatu na kutoka sare tatu. Kipigo cha mwisho ni mechi yao ya kufungia msimu ilipigwa mapema mwaka huu na Meddie Kagere kufanya yake dakika ya 71.

Hata kama akipoteza ubingwa kisha akaifunga Simba anaweza kujikuta anakuwa katika mikono salama.

Kutokana na hilo ni wazi Katibu Mkuu huyu atakuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha Yanga safari hii inafanya kweli na kuizima Simba ili kufuta uteja, vinginevyo huenda akajiweka kwenye wakati mgumu kama Jangwani watalala tena kwa Wekundu wa Msimbazi.

Ubingwa Ligi, Kombe la FA

Endapo Simba itachukua ubingwa msimu huu itakuwa ni mara ya tatu mfululizo, hii itakuwa sio habari njema kwa Yanga na Ruhago katika utawala wake hasa msimu huu hataweza kulikwepa kuhakikisha Yanga inarejea kuchukua ubingwa, Kombe la FA na hata timu yao kurejea kwa kishindo katika mashindano ya Afrika.

Yanga kukosa makombe yote hayo msimu huu itamfanya Ruhago kukosa usingizi na wakati wowote presha inaweza kuwa kubwa kutegemea na timu hiyo aliyonayo na kiu waliyonayo wanachama na mashabiki wa klabu hiyo.

Ruhago amepewa Yanga ikiwa nafasi ya 15 baada ya kushuka uwanjani mechi 5 ikikusanya alama 10, ikiwacha alama 12 na watani zao Simba wanaoongoza msimamo wakiwa na apointi 22 baada ya kucheza mechi tisa mpaka sasa.

Katibu huyo alipotafutwa jana ili kuelezea juu ya uteuzi wake na mambo ambayo anaenda kukabiliana nao Jangwani, alishindwa kutoa ufafanuzi kwa madai alikuwa safarini kwenda kwenye msiba uliompata.