Siri ya kambi ya Serengeti hii hapa

Muktasari:

  • Tayari nembo ya mashindano hayo imezinduliwa wakati vikao mbalimbali vya kamati ya maandalizi vikiendelea.

Dar es Salaam. Timu ya Taifa Tanzania chini ya miaka 14 (Serengeti Boys) imeweka kambi mkoani Arusha wakijiandaa na Mashindano yaliyoandaliwa na Uefa yatakayofanyika nchini Uturuki mwezi huu.

Serengeti Boys ambayo watakua wenyeji wa mashindano ya Afcon ya vijana chini ya miaka 17 yatakayofanyika nchini mwezi wa Aprili.

Kocha Oscar Milambo wa Serengeti Boys alisema wamechagua kambi hiyo ili wachezaji wake waweze kuanza kuzoea hali ya hewa ya baridi kabla hawajatimkia Uturuki.

“Arusha hali ya hewa ni baridi na watoto kwenye wiki mbili mbele wataondoka kwenda Uturuki ambapo hali ya hewa ni baridi, kwahiyo tumetaka kuzoea mazingira mapema,” alisema.

Oscar aliongeza kwamba morali ya wachezaji kambini hapo ni nzuri na wamekuwa wakifanya mazoezi kwa kufata programu kamili ili kufikia lengo wanalotaka.

Katika kambi hiyo imewajumuisha wachezaji 31 ambao wanajiandaa na Mashindano ya Afcon yatakayofanyika nchini, pamoja na UEFA Assist yatakayozikutanisha timu 8 za Afrika na 4 za Ulaya.