Soka la Kelvin John lamgusa dogo wa Nigeria aliyeko Chelsea

Dar es Salaam. Nyota ya mshambuliaji Kelvin John wa timu ya Taifa Tanzania chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ imezidi kung’ara baada ya mchezaji huyo kuonyesha uwezo mkubwa katika fainali za Afcon zinazoendelea nchini.

Kiwango ambacho amekionyesha katika michezo miwili imemfanya mchezaji wa U-17 ya Nigeria, Adrian Akande anayecheza katika kikosi cha Vijana Chelsea FC na timu ya Taifa Nigeria (U17) kuvutiwa na uchezaji wake.

Akande aliliambia Mwanaspoti kwa haraka haraka mchezaji ambaye anaweza kucheza hata Uingereza ni Kelvin John kutokana na uwezo wake mkubwa wa kumiliki mpira na kupambana na mabeki.

“Yule anayevaa jezi namba 10 ni mzuri anapopata mpira anajua afanye jambo gani, ana uwezo mkubwa sana wa kukaa nao lakini hata hatua anazopiga akiwa na mpira naa kutoka mabeki wa timu pinzani anaonyesha kabisa kwamba amekomaa, anaweza kucheza sehemu yoyote ile, napenda jinsi ambavyo anacheza,” alisema.

Aliongeza kupitia Fainali ambazo zinafanyika nchini mchezaji huyo anaweza akapata soko zuri la kukipiga katika klabu yoyote ile kama akiendelea na moyo wa kujituma kama ambavyo anafanya hivi sasa.

Kelvin katika Fainali hizi ameonyesha uwezo mkubwa katika safu ya ushambuliaji akiwa amefunga goli moja huku pacha wake Edmund John akiwa amefunga magoli mawili.