Stars hii Cape Verde wajipange

Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta (katikati), akiwania mpira na wachezaji wa timu hiyo Shomari Kapombe (kushoto) na Hassani Kessy, katika mazoezi yaliyofanyika jana mjini Praia, Cape Verde. Picha na Edo Kumwembe

Muktasari:

  • Timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ leo usiku inacheza na Cape Verde katika mchezo wa kufuzu Fainali za Kombe la Afrika zinazotarajiwa kufanyika nchini Cameroon.
  • Mara ya mwisho Taifa Stars kufuzu fainali hizo ilikuwa mwaka 1980, katika mashindano yaliyofanyika mjini Lagos, Nigeria.

Praia, Cape Verde. Kuna wakati mashabiki wa soka walikuwa wakitegemea miujiza kufuzu kucheza fainali za mashindano makubwa, kuna wakati walitegemea uwezo wa kocha, lakini leo watakuwa wakitegemea uwezo wa wachezaji na timu kwa ujumla watakapowavaa wenyeji Cape Verde kwenye Uwanja wa Taifa hapa Praia.

Mechi hiyo ya Kundi L itachezwa kuanzia saa 2:00 usiku na inaweza kuanza kutoa picha ya mustakabali wa kundi kupata timu zitakazofuzu kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani.

Baada ya kufuzu kucheza fainali za mashindano hayo mwaka 1980 wakati huo yakiitwa Kombe la Mataifa Huru ya Afrika, Tanzania haikuweza kupata fomula ya kurudia mafanikio hayo. Majaribio yaliyofuata baada ya hapo yalikuwa ni mbinu za kubahatisha na kusubiri miujiza.

Lakini baada ya mabadiliko ya uongozi, Kocha Marcio Maximo alileta matumaini mapya. Nchi sasa ikawa imeelekeza macho yake kwa Mbrazili huyo aliyerejesha mapenzi kwa timu ya Taifa.

Hata hivyo hakuweza kufanikiwa pamoja na matarajio ya Watanzania kuendelea kuwa kwa makocha, bado warithi wake raia wa Uholanzi Jan Poulsen, Kim Poulsen na Salum Mayanga hawakuweza kufuzu.

Katika kipindi cha makocha hao walizalishwa nyota ambao leo wameleta matumaini mapya kwa Watanzania.

Mbwana Samatta, Simon Msuva, Aishi Manula, Frank Domayo, Himid Mao, Thomas Ulimwengu, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, John Bocco ni baadhi ya wachezaji ambao wamebadili mtazamo wa wapenzi wa soka.

Ukiacha Nyoni na Domayo. Waliosalia watashuka dimbani leo kutafuta pointi muhimu za ugenini zitakazoimarisha nafasi ya Stars kwenye kundi lake.

Samatta anaongoza kundi hilo na anaingia kwenye mechi ya leo akiwa katika kiwango cha juu baada ya kufunga mabao matatimatatu mara mbili kwenye michuano tofauti akiwa na klabu yake ya Genk ya Ubelgiji inayoshirimi michuano ya Kombe la Europa ambayo ni ya pili kwa ukubwa kwa klabu barani Ulaya.

Msuva, ambaye anasakata soka Afrika Kaskazini, pia amekuwa mkombozi wa klabu yake, akiifungia mabao muhimu.

Mwingine ni Thomas Ulimwengu anayecheza nchini Sudan, Hassan Kessy (Zambia) na Mao anayechezea Petro ya Angola.

Sehemu kubwa ya nyota hao na wengine walioko Stars ni matunda ya programu za vijana.

Hakutarajiwi kuwa na mabadiliko makubwa katika kikosi cha emmanuel amunike baada ya kikosi chake cha awali kuonyesha uwezo mkubwa kilipolazimisha sare na Uganda mjini Kampala katika mechi yake ya pili katika michuano hiyo na kuifanya Stars kuwa na pointi mbili kutokana na kulazimishwa sare na Lesotho katika ya kwanza jijini Dar ed salaam.

Hakuna shaka kwamba samatta, ambaye ni nahodha wa timu ataongoza mashambulizi akisaidiana na Ulimwengu, mshambuliaji mwenye nguvu na bidii, huku wakisaidiwa na msuva.

Katika kiungo kunaweza kuwa na mabadiliko kutokana na kutokuwepo kwa domayo ambaye alipangwa katika mechi iliyopita na Mao kuingia baadaye katika kipindi cha pili. Amunike atalazimika kufanya uamuzi wa kuanza na nani kati ya mao na Feisal wakati mudathir anaonekana kujihakikishia nafasi katika sehemu ya mbele ya kiungo.

Katika mechi iliyopita, yondani halkusafiri na timu na hivyo Amunike akamtumia Aggrey Morris, David Mwantika na Abdi Banda katikati ya ngome ya stars huku kessy na gadiel wakimalizia safu ya kumlinda kipa Manula.

Samata alifunga bao la kuongoza katika mechi ya kwanza dhidi ya Lesotho ambao baadaye walisawazisha na kuizua Stars kupata ushindi nyumbani. Na hakionekani kikwazo cha kumzuia mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba kuendeleza moto wake ambao umezifanya klabu kubwa kama Everton kuanza kutaka wino wake.

Wachezaji wengi walioongea na vyombo vya habari juzi na jana wameshidi kucheza kwa jitihada kubwa kuiwezesha stars kuibuka na ushindi.

Pengine ni kutokana na kuona timu imekamilika, Shirikisho la Soka (TFF) likaamua kumsafirisha nyota ws zamani wa Stars, Peter Tino na timu ili awahamasishe kuwa wanaweza.

“Nitaawaambia kuwa nataka wanipokee kijiti kwa kuwa wanaweza,” alisema mfungaji huyo wa bao lililoipa Tanzania tiketi ya kucheza fainali za Afrika mwaka 1979 mjini Ndola, Zambia.

“ Si kwamba nataka wavunje rekodi yangu, la. Hawawezi kuvunja rekodi yangu kwa kuwa sisi ni kama timu moja ya mbio za kupokezana vijiti. Kwa hiyo nimeanzisha na sasa wakati umefika nataka wanipokee.”

Juzi kocha alitumia muda mwingi kufanya mazoezi kwenye uwanja mdogo, ikimaanisha anataka wachezaji wajiandae zaidi kwa mchezo wa pasi, uwezo wa kutafuta mpira kwa kushinikiza wapinzani, na uharaka wa kufanya maamuzi.

Stars imekuwa ikisumbuliwa sana na makosa katika kiungo na mipira ya krosi, lakini katika mechi mbili zilizopita hawakuonyesha udhaifu huo.

Wenyeji pia wamekuwa katika hali nzuri kimchezo. Walitoka sare ya bila kufungana na andora ya barani ulaya mwezi juni huku wakiibamiza Algeria kwa mabao 3-2 ugenini katika mechi za kirafiki.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya hapa, Cape Verde inaweza kuwakosa nyota wake wawili; kiungo Marco Soares anayechezea Feirense ya Ureno na Fernando Varela anayechezea klabu ya PAOK ya Ugiriki ambao ni majeruhi.

Kwa mujibu wa shirikisho la soka la hapa, hali ya Marco Soares inaendelea vizuri na Fernando Varela aliyeumia Jumatatu wakati akiichezea klabu yake ya PAOK hataweza kucheza mechi ya leo na ya marudiano.

Cape Verde ilianza mazoezi oktoba 8 na siku iliyofuata asubuhi ilikuwa maalumu kwa ajili ya kupima afya za wachezaji.

Stars ambayo ilikuja hapa kwa kutumia ndege ya kukodi, itaondoka ijumaa mara baada ya mechi na kutua Dar es salaam jumamosi alfajiri tayari kwa mechi nyingine dhidi ya cape verde itakayofanyika oktoba 16 kwenye Uwanja wa Taifa.