TPBRC: Mwakinyo hajaporomoka, ni tatizo la ‘kiufundi’

Dar es Salaam. Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Hassan Mwakinyo ana nafasi ya kupumua baada ya Kamisheni ya Kusimamia na Kuratibu Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), kusema kuwa kushuka hadi nafasi 86 kumetokana na kompyuta ya mtandao wa Boxrec kuingiza taarifa kimakosa.

Juzi, Watanzania waliamka na taarifa za mwanamasumbwi huyo aliyejizolea sifa nchini katika siku za karibuni kuporomoka kwa kiwango kikubwa katika msimamo wa mabondia wa kulipwa duniani na hivyo kutishia fursa mbalimbali ambazo angezipata.

Mwakinyo, bondia namba moja nchini kwenye uzani wa super welter aliorodheshwa kimakosa kuwa ameporomoka kutoka nafasi ya 24 hadi 86 huku wadau wa ngumi za kulipwa wakidai chanzo cha anguko hilo ni kutopigana muda mrefu.

Bondia huyo alipanda hadi nafasi ya 16, Septemba 8, 2018 alipomchapa Sam Eggington kwa TKO nchini Uingereza kabla ya kuporomoka hadi ya 24 kisha 86.

Katibu mkuu wa TPBRC, Yahya Poli alisema jana kuwa mara baada ya kuona Mwakinyo na mabondia wengine wameshuka viwango isivyo kawaida, waliwasiliana na Boxrec kujua chanzo cha viwango hivyo.

Poli alisema kuwa wamepokea taarifa kutoka Boxrec ikiwahakikishia kuwa orodha ya viwango hivyo si sahihi kutokana na makosa yaliyofanyika, na tatizo hilo siyo kwa mabondia wa Tanzania tu, bali ni dunia nzima.

Alisema mabondia wa Tanzania wanatakiwa kutohamaki kwani tatizo hilo siyo mara ya kwanza linatokea kwa kuwa miaka ya nyuma lilitokea pia kwa Abdallah Pazi maarufu Dulla Mbabe.

“Naomba Mwakinyo na mabondia wengine wachukulie tatizo hilo ni la kawaida kwa ulimwengu wa sasa, linatokea hata kwenye benki mbalimbali, lakini hufanyiwa marekebisho na kurejea katika hali ya kawaida,” alisema.

Alisema kuwa moja ya sababu iliyowafanya kuhoji Boxrec kuhusu orodha hiyo ya viwango ni hali ya sasa ambapo michezo mingi haifanyiki kutokana na tatizo la ugonjwa wa corona.

“Kama hakuna kinachoendelea katika michezo, kwa nini mabondia wengine wapande na wengine washuke wakati hawajashiriki katika michezo yoyote” alisema Poli.

Hivi karibuni, Mwakinyo aliporomoka hadi nafasi ya 24 kabla ya juzi kutangazwa kushuka maradufu na kutajwa na mtandao wa ngumi wa dunia (boxrec) kuwa bondia wa 86 kati ya 1,806 duniani huku akiendelea kusalia nafasi ya kwanza kati ya mabondia 21 nchini katika uzani wake.