Taifa Stars kufungua Afcon na Senegal ya Mane kufunga na Algeria ya Mahrez

Monday April 15 2019

 

Dar es Salaam. Mambo ni mengi muda mchache! Watoto wa mjini wanasema hivyo wakati TFF na Bodi ya ligi wakijuliza namna viporo vya Simba vitakavyopagwa, tayari CAF imetangaza ratiba ya mechi za Makundi ya Fainali za Mataifa ya Afrika 2019, Misri.

Katika ratiba hiyo Tanzania imepangwa Kundi C pamoja na Senegal, Algeria na Kenya na mechi zote za kundi hilo zitachezwa kwenye viwanja viwili ule wa Cairo na Uwanja wa Al-Salam unaomilikiwa na Jeshi Anga la Misri.

Taifa Stars itaanza harakati zake za katika mashindano ya Afcon 2019 kwa kuwavaa Senegal katika mchezo wa ufunguzi wa Kundi C Juni 23 kwenye Uwanja wa Cairo.

Baada ya mchezo huo vijana wa Emmanuel Amunike watarudi uwanjani Juni 27 kuwavaa majirani zao Kenya katika mchezo unaotegemewa kuwa na upinzani mkali kila timu ikitaka ushindi ili kujiweka vizuri katika kundi hilo.

Tanzania itacheza mechi yake ya mwisho ya Kundi C kwa kuwavaa Algeria Julai Mosi katika mchezo unaotegemewa kuwa na ushindani wa aina yake kutokana na rekodi ya timu hizo kila zinapokutana.

Tanzania ipo nafasi 131 katika orodha ya viwango vya Fifa ikiwa Kundi C pamoja na Algeria, Kenya na Senegal.

Kwa kupangwa na Senegal, maana yake Stars itakutana na nyota wa Liverpool, Sadio Mane lakini pia watakuwa na kibarua mbele ya Algeria ambayo inaongozwa na mshambuliaji wa Manchester City, Riyad Mahrez na pia ikumbukwe kwamba Kenya itakuwa chini ya uongozi wa nyota wa Tottenham Hotspurs, Victor Wanyama.

Timu hizo zote zimeshawahi kukutana na Stars kwa nyakati na mashindano tofauti lakini kati ya hizo zote, imecheza idadi kubwa ya michezo na Kenya ambayo inatoka nayo kwenye ukanda mmoja wa Afrika Mashariki na Kati.

Stars ilikutana na Senegal mara mbili mwaka 2007 katika kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika ambapo katika mchezo wa kwanza ugenini huko Dakar, Senegal ilichapwa mabao 4-0 na mchezo wa marudiano jijini Mwanza, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Algeria ndio pengine ni timu ambayo iliacha kumbukumbu mbaya kwenye soka la Tanzania baada ya kuichapa Stars mabao 7-0 mwaka 2015 katika mchezo wa marudiano wa kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia uliochezwa huko Bilda nchini Algeria baada ya timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2 kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa jijini Dar es Salaam.

Timu ya Tanzania inaundwa na wachezaji wanaocheza soka nje hasa barani Ulaya na Afrika.

Nyota wa timu hiyo ni mshambuliaji Mbwana Samatta anayecheza KRC Genk (Ubelgiji). Tanzania pia na wachezaji wengine wanaocheza Ulaya wakiwemo Shaban Chilunda na Farid Musa (Tenerife, Hispania).

Wachezaji wengine wa Tanzania wanaocheza soka barani Afrika katika nchi za Morocco (Simon Msuva), Misri wapo (Himid Mao, Yahya Zaid na Shiza Kichuya), Algeria yupo nyota mmoja anayecheza JS Saoura, Thomas Ulimwengu.

Botswana yupo Rashid Mandawa na Zambia beki Ramadhan Kessy. Hata hivyo nusu ya wachezaji wa Tanzania wanatoka katika kikosi cha Simba, Yanga na Azam.

Ratiba ya Kundi C

Juni 23: Senegal - Tanzania

Juni 23: Algeria - Kenya

Juni 27: Senegal - Algeria

Juni 27: Kenya - Tanzania

Julai 1: Kenya - Senegal

Ratiba kamili Makundi AFCON 2019: 

IJUMAA Juni 21

 - MISRI-ZIMBABWE [kundi A]

Jumamosi Juni 22

- RD CONGO-UGANDA [kundi A]

- NIGERIA-BURUNDI [kundi B]

- GUINEA-MADAGASCAR [kundi B]

Jumapili, Juni 23

- MOROCCO-NAMIBIA [kundi D]

- SENEGAL-TANZANIA [kundi C]

- ALGERIA-KENYA [kundi C]

 Jumatatu Juni 24

- IVORY COAST-AFRIKA KUSINI [kundi D]

- TUNISIA-ANGOLA [kundi E]

 - MALI-MAURITANIA [kundi E]

Jumanne, JUNE 25

- CAMEROON-GUINEA-BISSAU [kundi F]

- GHANA-BENIN [kundi F]

Jumatano JUNE 26

- NIGERIA-GUINEA [kundi B]

- UGANDA-ZIMBABWE [kundi A]

- MISRI-DR CONGO [kundi A]

Alhamis JUNI 27

MADAGASCAR-BURUNDI [kundi B]

 SENEGAL-ALGERIA [kundi C]

- KENYA-TANZANIA [kundi C]

Ijumaa JUNI 28

- TUNISIA-MALI [kundi E]

- MOROCCO- IVORY COAST [kundi D]

- AFRIKA KUSINI-NAMIBIA [kundi D]

Jumamosi JUNI 29

- MAURITANIA-ANGOLA (kundi E]

- CAMEROON-GHANA [kundi F]

- BENIN-GUINEA-BISSAU [kundi F]

Jumapili JUNI 30

MADAGASCAR-NIGERIA [kundi B]

- BURUNDI-GUINEA [kundi B]

- UGANDA-MISRI [kundi A]

- ZIMBABWE-RD CONGO [kundi A]

 Jumatatu, JULAI 1,

AFRIKA KUSINI- MOROCCO [kundi D]

- NAMIBIA-IVORY COAST [kundi D]

- KENYA-SENEGAL [kundi C]

- TANZANIA-ALGERIA [kundi C]

Jumanne, JULAI 2

 - BENIN-CAMEROON [kundi F]

 - GUINEA-BISSAU-GHANA [kundi F]

- MAURITANIA-TUNISIA [kundi E]

- ANGOLA-MALI [kundi E]

Advertisement