Taifa Stars yaibua hofu mechi ya Sudan ugenini

Dar es Salaam. Wakati timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ ikijiandaa kwa mchezo wa kimataifa dhidi ya Sudan, safu ya ushambuliaji imeonekana kufifisha matumaini ya Watanzania kupata ushindi ugenini.

Taifa Stars itacheza dhidi ya Sudan mchezo wa kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa Afrika Kwa Wachezaji wa Ndani (Chan) Ijumaa wiki hii nchini humo.

Matokeo ya mechi sita za mwisho ilizocheza Taifa Stars hayatoi nafasi kwa timu hiyo kupata ushindi baada ya mchezo wa kwanza kufungwa bao 1-0 na Sudan mjini Dar es Salaam.

Katika mechi sita ilizocheza, Taifa Stars imepata mabao mawili ndani ya dakika 90 hatua inayoashiria matumaini ya kufanya vyema Ijumaa ni madogo.

Timu hiyo ilitoka sare ya bao 1-1 na Burundi katika mechi zote mbili za kufuzu Fainali za Afrika kabla ya kushinda kwa penalti 3-0 ziliporudiana.

Pia ilitoka suluhu na Kenya kabla ya kushinda 4-1 katika mchezo wa Chan kabla ya kufungwa na Sudan 1-0 na juzi ilitoka suluhu dhidi ya Rwanda.

Ubutu wa safu ya ushambuliaji unaonekana kuitafuna Taifa Stars katika mechi zake za mashindano ingawa mara kadhaa Kocha Etienne Ndayiragije alikaririwa akisema atatumia viungo kupata mabao.

Kitendo cha kuita idadi kubwa ya wachezaji wa viungo kilionyesha dalili mbaya kwa timu hiyo kupata matokeo mazuri dhidi ya wapinzani wake.

Katika mchezo wa juzi, Ndayiragije aliwaanzisha Saimon Msuva na Adi Yusuf wanaocheza soka la kulipwa nje katika safu ya ushambuliaji. Wachezaji hao hawatacheza dhidi ya Sudan.

Mchambuzi Ally Mayay alisema alitarajia Ndayiragije kutoa nafasi kwa wachezaji wa ndani kwa kuwa ndio wataikabili Sudan kuliko akina Msuva na Yusuf.

“Kila kocha ana malengo inawezekana kwasababu za Afcon, Chan na dunia zinazoikabili Stars akaandaa Plani A na B. Alioanza nao huenda ilikuwa B na A ni ile aliyomaliza ya wazawa,”alisema Mayay.

Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Charles Mkwasa alisema kutokana na mazingira yalivyo, timu hiyo inapaswa kucheza soka ya kufunguka ili kupata mabao, lakini wanatakiwa kuchukua tahadhari katika safu ya ulinzi.

Mkwasa alisema wachezaji wa kiungo wamebeba matumaini ya kocha katika mchezo huo kwa kuwa pasi zao za mwisho zitakuwa na faida kwa washambuliaji.