Taifa Stars yanoa makali kwa Rwanda leo

Muktasari:

Mchezo huo ambao utachezwa Kigali, ni wa pili kwa Taifa Stars kucheza tangu Januari ya mwaka huu, mchezo wa kwanza ulikuwa Juni 13 dhidi ya Misri, ambao ulikuwa sehemu ya kujiandaa na fainali za mataifa ya Afrika ‘Afcon’.

Dar es Salaam.  Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’  leo itashuka uwanjani kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Rwanda ikiwa ni sehemu ya kujiandaa  na  mchezo dhidi ya   Sudan kuwania nafasi ya kufuzu kwa fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani   ‘CHAN’.

Kwa mujibu wa kaimu kocha mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije  alisema atatumia mchezo huo, kufanyia kazi baadhi ya mbinu ambazo kwa kushirikiana na  wenzake  anaamini zitawasaidia kufanya vizuri  katika mchezo wa marudiano dhidi ya Sudan.

Taifa Stars ilipoteza mchezo wa kwanza nyumbani kwa kufungwa bao 1-0, watacheza mchezo wa marudiano na Sudan, Ijumaa ya Oktoba 18.

“Nafasi yetu kucheza CHAN bado ipo wazi pamoja na kuwa tulianza vibaya mchezo wa kwanza, tuna wachezaji wenye uwezo mkubwa hivyo ni vyema mashabiki wa Tanzania wajivunie hilo, sidhani kama inashindikana kuwafunga Sudan.

“Kilichopo mbele yetu ni mchezo wa kirafiki, ambao kwa kiasi kikubwa utatusaidia kuwajenga wachezaji wetu kabla ya kucheza na Sudan, Rwanda wanatimu nzuri ambayo itatupa changamoto nzuri ya ushindani,” alisema.

Changamoto kubwa ambayo ilionekana katika kikosi cha Taifa Stars kwa wachezaji wa ndani ni namna ya umaliziaji kitu ambacho Etienne na wasaidizi wake Juma Mgunda na Seleman Matola wamekuwa wakikifanyia kazi.

Katika michezo miwili ya awali, Taifa Stars ilishindwa kupata bao mbele ya Kenya licha ya kusonga mbele kwenye hatua hiyo kwa mikwaju ya penalti baada ya kutoka suluhu kwenye michezo yote miwili, nyumbani na ugenini.

Katika moja ya mahojiano yake, Etienne aliwahi kukaririwa akisema anaitengeneza Taifa Stars kuwa na wigo mpana wa wachezaji wake kufunga hata wale ambao wamekuwa wakicheza kwenye  maeneo  tofauti na ushambuliaji.

Nyota wa kimataifa wa Tanzania, Saimon Msuva alisema bila shaka katika mchezo huo, wachezaji wa ndani watapata nafasi ya kutosha ili kuendelea kujengwa kwa ajili ya mipango ya kutumika kwenye mchezo dhidi ya Sudan.

“Kupata mchezo wa kirafiki kipindi hiki ambacho mbele kuna mchezo muhimu wa CHAN ni faida kwetu, mwalimu ataona wapi ambapo anaweza kupafanyia maboresho,” alisema Msuva anayeichezea Difaa El Jadida ya Morocco.

Pia, Msuva alisema mbali na kuutumia mchezo huo kama sehemu ya maandalizi ya  mchezo dhidi ya Sudan, ni muhimu  kuibuka na ushindi ili kuona kama wanaweza kusogea kwenye viwango vya ubora   wa soka duniani.

Erasto Nyoni ambaye amekuwa akitegemewa kwenye kikosi hicho hasa katika idara ya ulinzi, alisema wataipeperusha vyema bendera ya Tanzania kwenye mchezo huo wa kirafiki.

“Ushindi utatuweka katika nafasi nzuri ya kucheza mchezo wa marudiano dhidi ya Sudan, inawezekana kuwafunga hata kama ikiwa ugenini mbona wao waliweza kutufunga kwetu,” alisema.

Mara ya mwisho kwa Sudan kupoteza ilikuwa Machi 22 mwaka huu, walipokea kipigo cha mabaon 4-1 wakiwa nyumbani kutoka kwa Equatorial Guinea katika mchezo wa kuwania nafasi ya kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika 'Afcon'.