Taifa Stars yashikilia kibarua kocha Lesotho

Friday November 9 2018

 

Dar es Salaam. Mchezo wa  Taifa Stars na Lesotho, umemuweka pabaya Kocha Moses Maliehe anayekabiliwa na presha kubwa kutoka kwa vyombo vya habari nchini humo.

Taifa Stars na Lesotho zitamenyana Novemba 18 katika mchezo wa kuwania nafasi ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika, zilizopangwa kuchezwa mwakani Cameroon.

Maliehe amejikuta katika mazingira magumu baada ya kushambuliwa na vyombo vya habari kufuatia  Lesotho kuboronga kwenye michezo miwili iliyopita dhidi ya  Uganda.

Kwa mujibu wa mtandao wa  thepost.co.ls, Maliehe ana wakati mgumu baada ya kuwaita wachezaji wawili  katika kikosi chake dhidi ya Uganda kipa Mohau Kuenane na kiungo Jane Tsotleho ambao hawana timu.

Lesotho ilipoteza mchezo wa kwanza Oktoba 10 baada ya kulala mabao 3-0 jijini Kampala na siku sita baadaye ikiwa  Maseru ilinyukwa 2-0, Oktoba 16.

Maliehe alisema mchezo dhidi ya Taifa Stars unaotarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Setsoto ni nafasi pekee kwao ya kuweka hai matumaini ya kufuzu fainali hizo.

Advertisement