Tambwe amtaja mrithi wa Zahera Yanga

Friday November 8 2019

 

YANGA bado iko mafichoni kujua nani wampe jukumu la kuingoza baada ya kuvunja benchi zima la ufundi, lakini mshambuliaji wao wa zamani Amissi Tambwe amesema wala hajashtuka na hatua hiyo, lakini akamtaja kocha anayestahili kazi hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti kutoka kwao Burundi, Tambwe alisema hiyo wala haina kikosi kibovu kama wengi wanavyodhani, lakini shida ipo katika mbinu za uwanjani.

Alisema baada ya kocha Mwinyi Zahera kuondolewa Yanga inatakiwa kutafuta mtu ambaye atakuwa muumini wa soka la kushambulia na siyo kujilinda.

“Yanga haina kikosi kibovu, kuna mambo yalikuwa yanakosewa hata sisi wengine ni vile tulikuwa na uzoefu, lakini mfumo uliokuwa unatumika msimu uliopita usingeweza kutupa mafanikio,” alisema Tambwe.

“Sasa viongozi watulie katika kutafuta kocha sahihi asije tena kocha mwenye mbinu za kujilinda muda wote wa mchezo, ugumu mkubwa ulikuwa hapo timu lazima icheze na iwe na mbinu mbadala.”

Mshambuliaji huyo anayeshikilia rekodi ya mapro wa kigeni waliocheza Tanzania kwa kufunga mabao mengi Ligi Kuu katika misimu yake sita akifunga 73, huku akinyakua tuzo ya Mfungaji Bora kwa misimu miwili ya 2013-2014 akiwa Simba na 2015-2016 akiwa na Yanga, pia alisema kocha anayekuja anatakiwa kuzingatia nidhamu kwa wachezaji na hivyo anapaswa kuwa mkali.

Advertisement

“Yanga haiwezi kucheza na timu ndogo ikaomba mpira uishe, tulikuwa tunateseka sana tofauti na miaka ya nyuma, lakini kama kocha akiwa mkali kwa nidhamu na mbinu nzuri itarudi enzi zake za kutamba,” alisema.

“Hatua nzuri ni kwamba maamuzi haya yamefanyika mapema wakati ligi haijaenda mbali, sasa wanachotakiwa viongozi ni kutuliza akili na kufanya maamuzi ya haraka kumpata kocha mpya.”

Katika hatua nyingine Tambwe aliushauri uongozi wa timu hiyo kutofanya haraka kuwatimua wachezaji ambapo jukumu hilo aachiwe kocha mpya ambaye atakuja kukiangalia kikosi na kutoa ushauri.

Alisema endapo viongozi wataanza kuwaondoa wachezaji huenda wakawaondoa wazuri ambao pengine walionekana hawafai kutokana na mfumo wa uchezaji kuwashinda.

“Wasifanye haraka kuondoa mchezaji yeyote.”

Advertisement