Tambwe awapa raha Yanga

Sunday February 15 2015

Mshambuliaji wa Yanga, Andrey Coutinho, kulia

Mshambuliaji wa Yanga, Andrey Coutinho, kulia akimtoka beki wa BDF XI, Othusitse Mpharitlhe wakati wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Picha na Said Khamis 

By Oliver Albert, Mwananchi.

Dar es Salaam. Mshambuliaji Amissi Tambwe aliwapa raha mashabiki wa Yanga baada ya jana kuifungia timu yake mabao mawili dhidi ya BDF XI ya Botswana iliyokuwa ikishangiliwa muda wote na mashabiki wa Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kelele hizo za mashabiki wa Simba waliokiuka pendelezo la rais wao, Evance Aveva juzi kuwa wataishangilia Yanga ikicheza vizuri, hata hivyo hazikumzuia Tambwe kufunga mabao hayo.

Mabao ya Tambwe ambaye amekuwa butu kwenye Ligi Kuu yalipishana kwa dakika 54, yameiweka Yanga kwenye nafasi nzuri ya kufuzu kucheza hatua inayofuata ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Tambwe aliyejiunga na Yanga msimu huu akitokea Simba alifunga bao la kwanza, dakika ya kwanza ya mchezo huo akiunganisha krosi ya Haruna Niyonzima aliyepigiwa kona fupi na Simon Msuva.

Bao hilo liliwazindua wachezaji wa Yanga walioendelea kufanya mashambulizi kwenye lango la BDF XI, dakika ya 5,9,16 na 17 kupitia kwao, Mrisho Ngassa, Tambwe na Msuva, lakini mabeki wa timu hiyo ya jeshi walikuwa makini kuondosha hatari langoni mwao.

Wanajeshi hao walifanya shambulizi la kwanza, dakika ya 18 kupitia kwa Vicent Nzombe, lakini shuti lake lilipaa juu kidogo ya lango la Yanga.

Dakika saba baadaye, Yanga walijibu shambulizi hilo, lakini kwa mshangao wa wengi, Tambwe akiwa na kipa Takudzwa Ndoro alipiga shuti lililopaa, akishindwa kumpasia mpira Ngassa aliyekuwa kwenye nafasi nzuri.

BDF XI nusura ipate bao dakika ya 43, lakini mpira uliopigwa na Nzombe tena uliokolewa kistadi na beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na kuwa kona tasa.

Dakika mbili kabla ya filimbi ya mapumziko, Kelvin Yondani alirejea uwanjani baada ya kuwa majeruhi alionyeshwa kadi ya njano kutokana na kumsukuma Master Masitara.

Yanga walianza kipindi cha pili kwa mashambulizi ya nguvu kwenye dakika ya 47 na 49, lakini washambuliaji wake hawakuwa makini kuzitumia nafasi hizo.

Kiungo Salum Telela alifanya kazi ya ziada kumzuia Nzombe aliyekuwa akielekea kufunga, dakika ya 54.

Dakika moja baadaye, Tambwe aliwainua tena mashabiki wa Yanga kwa bao akiunganisha kwa shuti kali pasi ya Ngassa aliyekuwa mwiba kwa mabeki wa BDF XI.

Yanga waliotawala kipindi cha pili walifanya mabadiliko kwa kumpumzisha Andrey Coutinho na nafasi yake kuchukuliwa na Kpah Sherman, dakika ya 70 na kufuatiwa na mabadiliko mengine ya kutoka kwa Tambwe na nafasi yake kujazwa na Jerry Tegete.

Kocha Hans Pluijm alisema baada ya mhezo huo kuwa walihitaji bao moja zaidi ili kujiweka vyema, lakini akaeleza kuwa ameridhishwa na kiwango cha wachezaji wake.

Vikosi

Yanga; Barthez, Twite, Oscar ,Cannavaro, Yondani, Telela, Msuva, Niyonzima, Tambwe, Ngassa, Coutinho.

BDF XI; Takudzwa Ndoro, Pelontle Lerole, Othusitse Mpharitlhe, Keleagtse Mugotsi, Mompat Thumazo, Mosha Gaolaolwe, Master Masitara, Bonolo Phuduhudu, Vicent Nzombe, Thato Ogopotse, Kabelo Seakanyeng.

Advertisement