Tamu, chungu uteuzi wa Taifa Stars

Thursday June 13 2019

 

By Charles Abel

Dar es Salaam. Ni fursa na heshima kwa mchezaji kuitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa kinachoshiriki mashindano ya kimataifa kama vile Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), lakini mambo hugeuka pindi anapokosa nafasi hiyo dakika za lala salama.

Ndivyo hali inavyoweza kuwa kwa nyota 23 walioteuliwa na benchi la ufundi kuunda kikosi cha Taifa Stars kitakachoshiriki AFCON, wakitokea katika orodha ya wachezaji 32 waliokuwemo katika timu ya awali kujiandaa na fainali hizo.

Wakati wachezaji 23 wakifurahia kuandika historia ya kushiriki fainali hizo kwa mara ya pili, hali inaweza kuwa ngumu kwa nyota tisa ambao watalazimika kurejea nyumbani na kuyashuhudia mashindano hayo kupitia luninga.

Wachezaji tisa watakaokosa AFCON baada ya kushindwa kupenya katika kikosi cha mwisho cha wachezaji 23 ni makipa Selemani Salula na Claryo Boniface, mabeki Abdi Banda na David Mwantika, viungo Fred Tangalu, Miraji Athumani na Shiza Kichuya na kinda Kelvin John ‘Mbappe’.

Kutemwa kwa wachezaji hao na uteuzi wa wenzao 23 haukutokea kwa bahati mbaya, bali ni matokeo ya tathmini ya kina iliyofanywa na Kocha Emmanuel Amunike katika kipindi chote kabla na wakati wa maandalizi ya timu hiyo kabla ya fainali hizo.

Banda anayecheza nafasi ya beki katika klabu ya Baroka ya Afrika Kusini huenda akawa ametibuliwa na ukosefu wa ufiti wa mechi jambo ambalo limechangiwa kwa kiasi kikubwa kutopata nafasi ya kutosha katika idadi kubwa ya mechi za timu yake huko Afrika Kusini.

Advertisement

Majeraha hayo yalichangia kumuweka nje Banda kwenye idadi kubwa ya mechi hasa za mzunguko wa pili na hata alipopona aliendelea kusugua benchi katika kikosi ambacho msimu uliopita alicheza mechi 15 tu za Ligi Kuu Afrika Kusini.

Pia haishangazi kuachwa mshambuliaji Shabani Chilunda ambaye hivi karibuni amevunja mkataba wake na CD Tenerife ambayo ilimtoa kwa mkopo CD Izarra inayoshiriki Ligi Daraja la Tatu Hispania.

Chilunda amepita kipindi kigumu Hispania kutokana na kutopata nafasi ya kucheza na kwa kudhihirisha hilo, katika msimu mzima amecheza michezo 10 tu ambapo mitatu akiwa na Tenerife tena akicheza dakika 28, wastani wa dakika tisa kwenye kila mechi huku saba akicheza Izarra kwa jumla ya dakika 103 sawa na wastani wa dakika 15 tu kwa mechi.

Kama ilivyo kwa Kichuya ambaye tangu alipojiunga na ENPPI ya Misri amecheza kikosi cha timu hiyo kwa mechi tatu tu jumla ya dakika 89 sawa na wastani wa dakika 30 katika kila mchezo.

Kukosa ufiti inawezekana pia ikawa ndiyo sababu ya kuenguliwa David Mwantika ambaye tangu beki Mghana Yakubu Mohammed apone majeraha, Azam imekuwa haimpi nafasi ya kucheza na kujikuta akisota benchi.

Ni jambo lisiloshangaza Amunike kutowaita Miraji na Tangalu wa Lipuli ambao ni wazi wanakosa uzoefu na walipenya katika kikosi cha awali kama sehemu ya kuwaandaa kwa ajili ya mpango wa baadaye wa timu kama ambavyo siyo jambo baya kwa Kelvin wa timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ na mwenzake wa chini ya miaka 20, Claryo.

Nidhamu na kujituma itakuwa silaha kwa mabeki Ally Mtoni ‘Sonso’ wa Lipuli na Vincent Philipo wa Mbao FC ambao licha ya kucheza timu za kawaida, wameendelea kuaminiwa na Amunike.

Ni kama ilivyotokea kwa Rashid Mndawa ambaye licha ya kutupiwa virago na Defence Force XI ya Botswana, atakuwemo katika AFCON sanjari na Adi Yussuf ambaye amejiunga na Blackpool ya Ligi Daraja la Pili England.

Kauli za wadau

Kocha wa zamani Yanga, Kenny Mwaisabula alisema uteuzi umezingatia masuala ya kiufundi na mbinu.

Pia alisema kuondolewa kwa Kelvin na Claryo hakuna tatizo kwa kuwa kitendo cha kuitwa na Amunike katika orodha ya kwanza ni jambo la kujivunia.

Mchambuzi wa soka Ally Mayay alisema ana amini Amunike ameangalia wachezaji ambao wanaweza kuendana naye.

Mayay amewataka nyota waliopata nafasi kufanya vizuri katika mashindano hayo na kufuta rekodi ya kutolewa katika hatua ya makundi miaka mwaka 1980.

Advertisement