Tanzania yateleza kuogelea

Wednesday July 31 2013

By Imani Makongoro, Mwananchi

Waogeleaji wa Tanzania wameanza vibaya mashindano ya dunia nchini Hispania baada ya kushindwa kufuzu kuingia hatua ya pili kwenye mchujo wa Butter fly mita 50 na free style mita 200.

Nahodha wa timu ya Tanzania, Hilal Hemed Hilal alikuwa wa kwanza kuaga kwenye mtindo wa Butter fly akitumia sekunde 28:25 kumaliza kupiga mbizi na kushindwa kuendeleza muda wake wa sekunde 27:62 aliotumia kwenye mashindano ya Afrika huko Zambia mwanzoni mwa mwaka huu.

Mtanzania mwingine, Ammaar Ghadiyali alifuata nyanyo hizo akitumia dakika  2:15:28 kumaliza mbizi za free style mita 200 muda uliomkwamisha kuingia katika hatua ya pili ya mashindano hayo.

Kesho Hilal kwa mara nyingine atashuka bwawani kujaribu nafasi ya mwisho ya kusonga mbele kwenye mtindo wa free style mita 50 katika bwawa la Piscina Municipal de Montjuic huko jijini Barcelona. Hata hivyo katika kundi lao Mtanzania huyo ana nafasi kubwa ya kusonga mbele kutokana na muda wa kufuzu wa wapinzani wake kwenye kundi hilo ambapo Hilal anashikilia namba 3.

Muogeleaji Nikles Christian wa Burundi ndiye anaongoza akiwa ametumia sekunde 25:12 akifuatiwa na Sultan Farhan wa Berlin aliyetumia sekunde 25:20 na Hilal ambaye ametumia sekunde 25:30 akiwa mbele zaidi kwa wenzake.

Advertisement