Timu Ligi Kuu zaihofia Simba kutetea ubingwa

Wednesday February 13 2019

 

By Bertha Ismail

Arusha. Bodi ya ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeahidi timu zote zitakuwa na michezo sawa kuanzia raundi ya 30.

 Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura amesema licha ya kukabiliwa na changamoto upangaji wa ratiba kutokana na muingiliano wa michuano mbalimbali, amesema watahakikisha michezo yote ya viporo inakamilika kabla ya kuanza kwa raundi ya 30.

 Wakati baadhi ya timu zikiwa zimecheza michezo 26, nyingine zina mechi 22, 23, 24 na 25, huku Simba ikivunja rekodi kwa kuwa na viporo 11 ikiwa imeshuka dimbani mara 15 tu Wambura amesema ligi itamalizika mwezi Mei kama ilivyopangwa.

 Kumekuwa na mjadala kuhusu ubora wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu kutokana na sintofahamu ya ratiba huku ligi hiyo ikiwa haina mdhamini.

 Aidha, idadi kubwa ya viporo kwa Simba imeibua maswali mengi kutoka kwa wadau, baadhi wakiwa na hofu ya kuandaliwa kwa mazingira ya kuisaidia timu hiyo kutetea ubingwa iliyotwaa msimu uliopita.

 Lakini hapana shaka kama Bodi ya ligi itahakikisha viporo vyote vinamalizika kabla ya kuanza kwa raundi ya 30, angalau itarejesha ushindani ulio sawa baina ya timu zinazowania ubingwa na hata zile zinazopigania kubaki Ligi Kuu.

Advertisement