Tshishimbi, Mapinduzi wamvulia kofia Morrison

Muktasari:

Morrison amejiunga na Yanga katika usajili wa dirisha dogo lililofungwa Januari 15, mwaka huu akiwa ni miongoni mwa mastaa wapya saba waliosajiliwa wengine ni Eric Kabamba, Adeyum Saleh, Tariq Seif, Ditram Nchimbi, Haruna Niyonzima na Yikpe Gislain.

Dar es Salaam.Wachezaji wa Yanga wamesifu kiwango kilichoonyeshwa na mshambuliaji wao mpya, Bernard Morrison uwepo wake ni chachu ya mafanikio.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wachezaji hao walisema tangu Morrison amejiunga na klabu hiyo ameonyesha uwezo mkubwa wa kuisaidia timu kupata matokeo.

Nahodha wa Yanga, Papy Tshishimbi alisema ni mchezaji anayejitambua na anajua namna ya kukaa eneo sahihi kwa wakati sahihi na kuweka wazi kuwa ujio wake umeongeza changamoto hasa kwa wachezaji wanaocheza nafasi yake.

"Anaisaidia na ataendelea kuisaidia Yanga kama atabaki na kiwango chake ambacho kimeweza kuwa imara akiwa bado ajazoeana na wachezaji aliowakuwa ni nadra sana kwa mchezaji kujiunga na timu na kuzoea mfumo kwa siku chache alizokaa kambini," alisema Tshishimbi.

"Ni mapema sana kuendelea kumsifu, lakini kikubwa watu wanatakiwa kutambua kuwa huyu ni mchezaji mwenye kipaji na si mchezaji wa kutumia nguvu nyingi kufanya mazoezi hivyo waendelee kumuamini na wategemee mambo mazuri zaidi kwa namna mimi nilivyomfuatilia," alisema nahodha huyo.

Naye Mapinduzi Balama alisema anashangazwa na juhudi zake mazoezini kabla ya kufika uwanjani kucheza mchezo wa ushindani kusaka pointi tatu muhimu huku akifichua siri nyingine kuwa wao wanamfaidi zaidi huko na sio uwanjani.

"Siku ya kwanza kufanya mazoezi pamoja sio mimi tu nadhani ni wachezaji wote walikoshwa na kiwango chake Morrison anajua kuchezea mpira anapiga pasi za uhakika ni mchezaji mzuri tunatarajia makubwa kutoka kwake."

Mapinduzi aliongeza kuwa kwa muda mchache waliokaa naye wamebaini kuwa sio mchezaji wa kufundishwa mbinu yeye anajua namna ya kucheza na akili ya kila mchezaji ni muda gani anatakiwa kukaa na mpira mguuni na muda gani atoe pasi kwa mchezaji mwenzake.