Twiga Stars kuendeleza ubabe Morocco leo

Muktasari:

  • Kikosi cha timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania 'Twiga Stars' inaingia uwanjani jioni hii kucheza na Morocco kwenye Uwanja wa Kram.

Dar es Salaam. Timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania 'Twiga Stars' leo Jumanne majira ya saa 9: 15 jioni, itaingia uwanjani kuivaa Morocco katika michuano ya iliyoandaliwa n Shirikisho ka Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Kaskazini (UNAF).
Twiga Stars imekuwa tishio katika mashindano hayo baada ya kushinda mechi mbili mfululizo ilipoichapa Mauritania mabao 7-0 pamoja na Algeria mabao 3-2.
Inatamba na  wachezaji wake nyota kama Zubeda Mgunda,  Mwanahamisi Omary 'Guacho', Asha Rashid 'Mwalala', Opa Clemence, Fatuma Khatib na Violeth Machela.
Mwanahamisi amesemea, imekuwa michuano mizuri kwao.
"Lengo ni kushinda mechi zote za kwenye michuano hii ambayo imekuwa kipimo kizuri kitakachotuimarisha mbele ya safari yetu. Morocco ni timu nzuri lakini tumejipanga kuwafunga,"alisema Mwanahamisi.
Twiga watacheza mechi hiyo baada ya mchezo wa Mauritania dhidi ya Algeria.
Mchezo huo, utapigwa kwenye Uwanja wa Kram ulio Tunis, Tunisia na ndio unatumika kucheza michezo yote ya mashindano hayo ya UNAF.
Jumla ya mataifa matano yameshiriki katika michuano hiyo ambayo ni Tanzania, Algeria, Mauritania, Morocco na wenyeji Tunisia na ilianza kutimua vumbi Februari 14 mpaka 23 na inachezwa kwa mtindo wa ligi.