Tyson Fury amkalisha Wilder raundi ya saba

Muktasari:

  • Kona ya Wilder ilirusha taulo katika raundi ya saba ya pambano hilo na kumfanya refa Kenny Bayless kuingilia kati na kumuokoa Wilder ambaye alikuwa anapokea ngumi mfululizo

LAS VEGAS, MAREKANI. Bondia Tyson Fury ametwaa mkanda wa uzito wa juu duniani wa WBC baada ya kumtwanga kwa TKO Mmarekani Deontay Wilder katika pambano la raundi 12 lililochezwa leo katika ukumbi wa MGM Grand Arena, Las Vegas, Nevada, Marekani.

The Gypsy King ambaye aliingia kwenye pambano hilo akiwa amevaa kifalme kwa ushindi huo  amempora Wilder mkanda wa WBC  na amefanikiwa kutwaa mkanda wa Ring Magazine ambao haukuwa na mwenyewe.

Fury bingwa wa zamani wa uzito wa juu wa WBA, WBO, IBF na IBO, alitawala pambano hilo na kumshambulia Wilder tangu kengere ya kwanza huku akimpa wakati mgumu Mmarekani huyo kutumia mkono wake wa kulia ambao umekuwa ukimpa ushindi.

Akionekana kubadilika zaidi kulinganisha na pambano la kwanza Fury alimkalisha Wilder mara mbili kabla ya kona ya Mmarekani huyo kuona inatosha na kurusha taulo kwenye raundi ya saba.

Kona ya Wilder ilirusha taulo katika raundi ya saba ya pambano hilo na kumfanya refa Kenny Bayless kuingilia kati na kumuokoa Wilder ambaye alikuwa anapokea ngumi mfululizo, lakini baada ya mwenyewe akadai kuwa bado alikuwa na uwezo wa kujilinda.

“Natamani timu yangu ingeniacha nijilinde.” Alisema Wilder ambaye anaamini watu wake walikatisha pambano mapema wakati bado alikuwa na uwezo wa kuendelea kupambana.

Ushindi huu wa Fury unaonekana kuchana mikeke ya watu wengi kwa sababu jijini Las Vegas kampuni za kubashiri zilimpa nafasi kubwa Wilder kushinda pambano hilo kutokana na historia yake.