Uchaguzi Yanga waingia dosari

Muktasari:

Mchungahela alifafanua kwamba uchaguzi umesitishwa baada ya baadhi ya wanachama kufungua kesi katika Mahakama Dar es Salaam, Mbeya na Morogoro.

Dar es Salaam. Kama mchezo wa kuigiza vile! Ndivyo ilivyokuwa jana muda mfupi kabla ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ally Mchungahela kutangaza kusitishwa Uchaguzi wa Klabu ya Yanga.

Mchungahela akiwa na Makamu wa Rais wa TFF, Athumani Nyamlani walitumia saa 2:30 wakiwa Ofisi Ndogo ya Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dar es Salaam jana kuweka mambo sawa kabla ya kufikia uamuzi wa kutangaza kusitisha mchakato huo.

“Tukiwa kwenye kikao cha mwisho cha maandalizi ya uchaguzi, tulipata taarifa kuhusu baadhi ya kesi kufunguliwa mahakamani kupinga, hivyo tumelazimika kusitisha mchakato wa uchaguzi uliokuwa ufanyike Jumapili hadi tutakapopokea oda ya Mahakama,” alisema Mchungahela kwa hisia.

Mchungahela alifafanua kwamba uchaguzi umesitishwa baada ya baadhi ya wanachama kufungua kesi katika Mahakama Dar es Salaam, Mbeya na Morogoro.

“Hatutaki kwenda kinyume na Mahakama, tumeamua kusitisha mchakato huo hadi tutakapopata oda ya mahakama, mchakato wa nini kitaendelea kuhusu uchaguzi huo itajulikana Jumatatu,” alisema Mchungahela.

Awali, kabla TFF kutangaza kusitisha uchaguzi, Mchungahela na Nyamlani walikutana wa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harison Mwakyembe katika kikao kilichohudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Alex Nkenyenge.

Uchaguzi wa Yanga ambao ni kujaza nafasi ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na baadhi ya wajumbe umekuwa kama mchezo wa kuigiza, baada ya awali Yanga kupingana na TFF na Serikali kabla ya pande hizo kufikia mwafaka na kampeni zilianza kabla ya kusitishwa.