Uefa yaweka kapuni mageuzi 'yaliyotishia kuua' ligi za Ulaya

Muktasari:

Kwa mujibu wa mageuzi hayo, ligi ingeanza kwa timu kupangwa katika makundi yenye timu nane na baadaye timu sita za juu kusonga mbele bila kujali nafasi zao kwenye ligi za nchi.

Chama cha Soka Ulaya (Uefa) jana Alhamisi kiliahirisha kwa muda usiojulikana kikao muhimu cha viongozi wakuu ambacho kingejadili mageuzi makubwa katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.
Mkutano huo ambao awali ulipangwa kufanyika Septemba 11 kwenye makao makuu ya chombo hicho mjini Nyon, kilitarajiwa kukutanisha viongozi wa Chama cha Klabu za Ulaya (ECA), viongozi wa ligi z Ulaya na wawakilishi kutoka sehemu mbalimbali za Ulaya.
Lakini katika barua iliyoonwa na AFP ambayo imetumwa kwa rais wa ECA, Andrea Agnelli, kiongozi wa Ligi za Ulaya na Lars-Christer Olsson iliyotumwa na rais wa Uefa Aleksander Ceferin, inasema "ameamua kuahirisha kikao cha Septemba 11".
"Kwa sasa tuko kwenye mchakato wa kukusanya maoni kutoka vyama vya soka vya nchi na nahisi –- kwa ujumla zaidi –- kwamba mazungumzo mapya sasa yatakuwa yamewahi sana kwa kuwa tunachambua maoni na mapendekezo kutoka pande tofauti," ameandika Ceferin.
Ceferin aliongeza kuwa "hakutegemea kufanya uamuzi nwowote mwaka huu" kuhusu mabadiliko katika mfumo wa mashindano ya klabu ya Ulaya kuanzia mwaka 2024, ambayo yalipendekjezwa na ECA na yamekumbana na mapingamizi.
Ilipoulizwa na AFP, Uefa ilisema tarehe mpya kwa ajili ya mkutano huo bado haijapangwa. Awali kikao hicho cha viongozi wakuu klilipangwa kufanyika siku moja baada ya mkutano mkuu wa ECA jijini Geneva.
Kuahirishwa kwa mkutano huo kumekuja huku kukiwa na hofu dhidi ya mapendekezo ya ECA yanayochagizwa na Agnelli, ya mashindano hayo kutawanywa katika madaraja matatu, kuwa yangeua ligi za nchi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa, ligi ya juu ingekuwa na makundi manne ya timu nane na timu sita kutoka katika kila kundi zikifuzu kucheza hatua inayofuata bila ya kujali nafasi ambazo timu hizo zimeshika katika ligi ya nyumbani.
Agnelli alitetea mpango huo akisema ni jaribio la kuziokoa klabu ndogo dhidi ya ligi tano kubwa.
Hata hivyo Ligi Kuu ya England, ambayo iliingiza timu nne katika fainali za Ligi ya Mabingwa na Kombe la Europa, imepinga pendekezo hilo kwe akauli moja.
Juni 15, klabu za Ligi Kuu ya Italia (Serie A) ambako kuna timu ya Agnelli ya Juventus iliyoshikilia ubingwa kwa takriban muongo mmoja, zilipinga pendekezo la mageuzi hayo, huku Juve ikiwa klabu pekee iliyounga mkono.
Klabu zilizopinga za Serie A, ambazo ni pamoja na Napoli na Lazio, zinaamini kuwa kuwa mpango huo unaweza kusababisha kupunguza mapato ya mechi za ligi hiyo kwa hadi asilimia 35.
Klabu saba za Hispania, lakini si Real Madrid wala Barcelona, pia zinapinga mpango huo sambamba na klabu za Ujerumani (Bundesliga), wakati timu 17 za Ufaransa pia zimepinga wakati Paris Saint-Germain, Lyon na Marseille hazijaweza misimamo yao.
Mwezi Mei, mtendaji mkuu wa Bayern Munich, Karl-Heinz Rummenigge aliponda mageuzi hayo, akisema tayari Ligi ya Mabingwa ni michuano bora duniani.