Uingereza ikijitoa EU, panga kupita kwa wachezaji England

Thursday March 14 2019

 

By Charles Abel

Nia ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May kuona nchi yake inajiondoa katika Umoja wa Ulaya (EU) imegonga mwamba na kesho Wabunge wa Uingereza watapiga kura ambazo dalili za awali zinaonyesha kuwa zitakuwa za kujiondoa kwenye Jumuiya hiyo.

Sababu hasa za kisiasa na kiuchumi ndizo zinaonekana zimechochea kiu ya kundi kubwa la raia wa Uingereza kutaka kuona wanajiondoa katika Umoja wa Nchi za Ulaya kwa kile wanachoamini kwamba hawanufaiki na uwepo wao kwenye Jumuiya hiyo tofauti na mawazo ya May.

Hata hivyo uamuzi kama huo unavyochukuliwa ni lazima uwe na faida na hasara, matokeo ambayo huenda sambamba ingawa yale yenye manufaa zaidi kwa mtazamo na hisia za wahusika ndio huchukuliwa.

Ikiwa Uingereza itajiondoa rasmi kwenye Jumuiya ya Ulaya, mchezo wa mpira wa miguu (soka) ambao ni moja ya utambulisho mkubwa wa visiwa vinavyounda nchi hiyo hasa England, ni miongoni mwa sekta zitakazopata athari hasi na uamuzi huo.

 

Inawezekana upande wa kisiasa na kiuchumi nchi hiyo ikanufaika lakini Ligi Kuu ya England (EPL) ambayo inatajwa kama Ligi Bora na maarufu zaidi ya soka duniani ukakumbana na anguko litakaloishusha hadhi na kutoa nafasi kwa ligi nyingine kama ile ya Hispania (La Liga), Ujerumani (Bundesliga), Italia (Serie A) na Ufaransa (Ligue One) kushika hatamu.

Advertisement

Makala hii inakuletea baadhi ya athari ambazo zitaikabili Ligi Kuu ya England baada ya nchi ya Uingereza kujiondoa kwenye Jumuiya ya Ulaya.

 

Kupungua kwa nyota wa kigeni

Kwa sasa kuna urahisi kwa nyota wengi wa soka kutoka  mataifa mbalimbali barani Ulaya kucheza Ligi Kuu ya England wakitumia mwavuli wa hati ya kusafiria ya Jumuiya ya Ulaya lakini pia kulegezewa masharti ya kupata vibali vya kazi nchini humo.

Nyota wengi wamekuwa wakipata urahisi wa kucheza kwa kutumia kanuni ya kuhesabika kama wachezaji wa nyumbani kutokana na kupitia kwenye vikosi vya vijana vya klabu zinazoshiriki ligi hiyo.

Lakini kwa sasa hilo halitokuwepo na wachezaji ili wacheze ligi nchini humo ni lazima watimize vigezo mbalimbali ambavyo vimewekwa kwa ajili ya kupata vibali vya kufanya kazi nchini humo.

Moja ya vigezo au masharti hayo ni namna mchezaji anavyopata nafasi katika timu yake ya taifa anakotokea. Ni lazima mchezaji awe ametoka katika nchi zilizopo kwenye nafasi 50 bora katika viwango vya ubora wa soka vinavyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).

 

Kwa mchezaji ambaye nchi yake ipo nafasi ya kwanza hadi ya 10, anapaswa angalau awe amecheza aslimia 30 za mechi za timu yake ya taifa na nchi zilizo nafasi ya 11 hadi 20 mchezaji anatakiwa kucheza 45% ya mechi za timu ya taifa.

Nafasi ya 21 hadi ya 30, mchezaji anatakiwa acheze 60% ya mechi za timu ya taifa na 75% ya mechi za timu ya taifa zinapaswa kuchezwa na mchezaji ambaye nchi yake iko nafasi ya 31 hadi ya 50 kwenye viwango vya ubora wa FIFA.

Kwa nchi ambazo haziko kwenye viwango 50 maana yake hatopata nafasi ya kucheza Ligi Kuu ya England.

Kwa mujibu wa Miles Jacobson ambaye ni Mkurugenzi wa Mahusiano ya Michezo wa England, ikiwa Uingereza itajitoa kwenye Jumuiya ya Ulaya, 25% ya wachezaji wa Ligi Kuu ya England ambayo ni takribani 152 watapoteza sifa za kucheza ligi hiyo.

 

Kuporomoka mvuto wa EPL

Ugumu wa wachezaji kutoka mataifa mengine kupata vibali vya kucheza ligi hiyo pamoja na mbinyo kwa wawekezaji ni wazi kwamba utapunguza umaarufu na mvuto wa ligi hiyo kwani utapunguza kasi ya mashabiki kuifuatilia na kuhamisha mahaba kwa ligi nyingine.

 

Kupungua kwa wawekezaji

 

Kwa sasa Ligi Kuu ya England imekuwa ikibebwa na Matajiri kutoka nchi mbalimbali duniani hasa zile za Asia ambao wamewekeza kiasi kikubwa che fedha.

Fedha za matajiri hao ndizo zimekuwa zikiziwezesha timu kusajili na kulipa mishahara ya mastaa mbalimbali wa soka kutoka nchi tofauti duniani.

Kujitoa kwa Uingereza maana yake kutasababisha mbinyo kwa wawekezaji hawa jambo linaloweza kuwakimbiza na kupelekea timu ziathirike kwa kushindwa kuwa na nguvu ya kiuchumi.

Advertisement