Ukarabati Jukwaa Kuu Uwanja wa Taifa umefika patamu

Wednesday March 13 2019

 

By Charles Abe

Dar es Salaam. Wakati mwezi mmoja ukibakia kabla ya kuanza kwa Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 zitakazofanyika hapa nchini, ukarabati wa Jukwaa Kuu la Uwanja huo unakaribia kukamilika.

Ukarabati huo umekuwa ukihusu uwekaji wa paa pamoja na viti katika eneo wanalokaa wageni na watu mashuhuri (VIP) uwanjani hapo.

Katibu mkuu wa kamati ya ndani ya maandalizi ya mashindano hayo, Leslie Liunda alisema mara baada ya ukarabati huo, utaratibu wa ukaaji kwenye eneo/jukwaa hilo utabadilika.

"Jukwaa kuu linafanyiwa marekebisho katika namna ambayo sasa hivi kutakuwa na takribani siti 72 tu na viti vyenyewe vitawekwa tofauti na zamani ambapo sasa mtu anapokaa atatazama mechi kwa vizuri tofauti na hapo mwanzo ambapo aliyekaa mbele anampa tabu aliye nyuma yake kutazama mechi vizuri.

“Pia sasa hivi pale Jukwaa Kuu sio kila kiongozi au Ofisa ataweza kukaa. Wataangaliwa wale wanaostahili zaidi kwa mujibu wa maelekezo tutakayopewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF)," alisema Liunda.

Liunda alisema ukarabati wa namna hiyo utahusu pia Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi ambao nao utatumika kwa mashindano hayo.

Jumla ya timu nane zitashiriki mashindano hayo ambazo ni wenyeji Tanzania 'Serengeti Boys', Uganda, Angola na Nigeria zilizo Kundi A pamoja na timu za Guinea, Cameroon, Morocco na Senegal zilizo Kundi B.

Advertisement