Utamu wa Taifa Stars, Uganda Cranes utakuwa hapa

Muktasari:

  • Tanzania inahitaji kushindi mchezo huo ili kupata tiketi ya kucheza fainali za Juni nchini Misri, pia ikiomba Lesotho ipata sare au kufungwa na Cape Verde

Dar es Salaam. Tanzania ‘Taifa Stars’ inahitaji ushindi dhidi ya Uganda Cranes wenye pointi 13, ili kufuzu kwa AFCON 2019.

Uganda tayari imefuzu kwa fainali hizo na kuiacha vita ya kupata timu moja ya kuungana naye kwa nchi tatu Tanzania, Lesotho naCape Verde.

Katika mechi hizo za mwisho leo itaamua hatma ya Tanzania na Lesotho zenye pointi tano kila moja na Cape Verde ikiwa na pointi nne.

Tanzania watakuwa wenyeji wa Uganda katika mchezo wenye ushindani wa aina yake kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Cape Verde watakuwa nyumbani kuwakaribisha Lesotho mjini Praia.

Mashabiki watakaokuwa uwanjani na wale watakaokuwa majumbani kuna maeneo yatakayokuwa na ushindani zaidi kati ya Tanzania dhidi ya Uganda leo jioni.

Mbwana Samatta (Tanzania) Vs Dennis Onyango (Uganda)

Kipa bora Afrika kwa sasa Dennis Onyango atakuwa na kibarua kizito cha kumzuia mshambuliaji mahiri kwa sasa Mbwana Samatta.

Kipa namba moja wa Mamelodi Sundowns ambaye ni nahodha wa Uganda Cranes atakuwa na lengo la kuendeleza rekodi yake nzuri dhidi ya mshambuliaji ya KRC Genk, Samatta wakati manahodha wakiwa jukumu la kuzibeba nchi zao.

Tayari, Onyango ameonyesha kuwa ni bora akiwa hajaruhusu bao lolote katika mechi tano za hatua ya makundi, atakuwa na lengo la kuendeleza rekodi yake.

Samatta ananjaa ya kutaka kuipa mafanikio Tanzania kwa kufuzu kwa fainali za Afcon kwa mara ya pili baada ya miaka 39.

Thomas Ulimwengu (Tanzania) Vs Murshid Jjuuko (Uganda)

Murushid Jjuuko atakuwa na kazi nzito mbele ya mshambuliaji wa JS Soura, Thomas Ulimwengu katika mchezo huo.

Ulimwengu ni mshambuliaji mwenye nguvu amekuwa akiwazidi nguvu mabeki kutokana na uwezo wake wa kukimbia na mpira.

Atakuwa na kazi nzito mbele ya Jjuuko ambaye amekuwa ni nguzo muhimu katika safu ya ulinzi ya Uganda Cranes, hali hiyo inafanya wawili hao kuwa katika vita ya hali ya juu.

Simon Msuva (Tanzania) Vs Godfrey Walusimbi (Uganda)

Ni winga wenye kasi Simon Msuva atakuwa na kibarua kizito mbele ya beki wenye akili nyingi Godfrey ‘Jjajja Walu’ Walusimbi.

Nyota huyo wa Difaa El Jaadid, anategemewa kuiongoza Taifa Stars kuhakikisha inapata ushindi.

Walusimbi ni mchezaji mzoefu anayejua vizuri kucheza na mawinga wenye kasi hivyo kunategemewa ushindani mkali kutoka pembeni mwa uwanja katika dakika 90.

Himid Mao (Tanzania) Vs Khalid Aucho (Uganda)

Mechi nyingi zinaamuliwa na vita ya katikati ya uwanja.

Himid Mao anayecheza Petro Jet ya Misri ataonyeshana kazi na kiungo Khalid Aucho anayecheza soka la kulipwa India katika klabu ya Churchhill Brothers.

Wachezaji wote wawili wanauwezo wa kupora mpira na kupiga pasi pamoja na kutawala vyema eneo la kati ya uwanja.

Mshindi wa vita ya katikati ya uwanja ndiye atakayetoa mwanya kwa timu yake kufanya vema.

Hassan Kessy (Tanzania) Vs Emmanuel Okwi (Uganda)

Dar es Salaam ni nyumbani kwa mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi.

Okwi amejijengea sifa na kupendwa zaidi na mashabiki kutokana na uwezo wake wa kufunga mabao katika Ligi Kuu Bara.

Hata hivyo, hakutakuwa na mapenzi leo kwa Okwi leo wakati atakapokuwa akicheza dhidi ya Taifa Stars.

Ni mchezaji muhimu katika mchezo huu hasa kutokana na uwezo wake wa kufunga mabao kwa mashuti ya mbali kutokea eneo lolote.

 Hata hivyo leo Okwi atakuwa chini ya ulinzi wa beki wa Hassan Ramadhan ‘Kessy’ anayecheza Nkana FC ya Zambia.

Kessy alitakuwa na jukumu moja la kuhakikisha Okwi hapati muda wa kucheza na mpira kama alivyokuwa amefanya wakati wa mchezo wa baina ya Simba na Nkana.

John Bocco (Tanzania) Vs Nico Wadada (Uganda)

Endapo Tanzania inataingia uwanjani kwa lengo la kushambulia zaidi hakuna ubishi kuwa wanaweza kuanza John Bocco, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.

Bocco anauwezo wa kufanya mashambulizi yake akitokea pembeni pia ni mzuri kwa kucheza mipira ya juu.

Kama atatokea kushoto atakutana na beki wa kulia wa Uganda Cranes, Nico Wadada anayechezea klabu ya Azam.