VIDEO: Kocha Mbelgiji Luc atua Dar es Salaam aifuata Yanga Zanzibar

Muktasari:

Mbelgiji Luc amekuwa na rekodi nzuri barani Afrika kwa klabu zake mbalimbali kufanikiwa kupata mataji katika nchi alizofundisha au kuziweka klabu zake katika mazingira mazuri katika misimamo ya ligi.

Dar es Salaam. Kocha mpya wa Yanga Mbelgiji Luc Eymael amewasili nchini mchana wa leo Alhamisi Januari 9, 2020 kuunganisha ndege moja kwa moja kwenda visiwani Zanzibar.

Mbelgiji Eymael aliwasili saa 9:24 alasiri akiwa na Meneja wa maendeleo wa GSM Hersi, baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam, hawakuwa na muda wa kupoteza moja kwa moja waliondoka kwenda Zanzibar.

Eymael alisema si mgeni hapa Tanzania nakuja kwa mara ya pili na nalifahamu vizuri soka la nchi hii kabla ya kuja kuomba kazi Yanga.

"Kwa nguvu ya wadhamini wa klabu, wachezaji na viongozi wote naimani ujio wangu utakuwa mzuri na nitafanya kazi katika mafanikio," alisema.

"Kuhusu timu nimeiona ilivyocheza mechi na Simba na kuna vitu vidogovidogo ambavyo nitaviongoza na mambo yatakuwa mazuri kutokana nimeona kuna wachezaji wengi wenye uwezo.

"Nakwenda Zanzibar kusaini mkataba ambao utakuwa na miezi 18, lakini nitaonana na wachezaji na kukabidhiwa timu na mambo mengine yataanza kuanzia hapo," alisema Eymael.

Mbelgiji Luc amekuwa na rekodi nzuri barani Afrika kwa klabu zake mbalimbali kufanikiwa kupata mataji katika nchi alizofundisha au kuziweka klabu zake katika mazingira mazuri katika misimamo ya ligi.

Mbali ya Leopards Mbelgiji huyo amewahi kufundisha klabu za Polokwane City na Free State Stars zote za Afrika Kusini.

Kocha Eymael alijenga heshima yake katika soka la Afrika Kusini baada ya kuibadilisha Polokwane kutoka kuwa timu ndogo na kuwa timu ya tishio kabla kutwaa ubingwa wa Kombe la Nedbank akiwa na Free State Stars 2017.

Mbelgiji Eymael ndiye aliyeviibua na kuvikuza vipaji vya nyota kadhaa wa Ubelgiji akiwamo Eden Hazard, Axel Witsel, Logan Bailly, Guillaume Gillet, Christian Benteke na François Sterchele.

Kocha Luc mwenye Leseni UEFA Pro na Leseni A ya CAF aliingia kufundisha soka la Afrika 2010 akiiongoza AS Vita kufika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa, pia aliweka rekodi ya kushinda mechi 23 za mashindano yote kabla ya kuachana na klabu hiyo Aprili 2011.

Mei 2011, alitimikia Gabon na kujiunga na klabu ya Missile ambayo aliiongoza kutwaa ubingwa wa nchi hiyo na mwaka 2012 aliweka historia kwa kuisaidia timu hiyo kufuzu kwa raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa pia kucheza hatua ya 16 bora wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Pia alisaidia wachezaji wengi wa kikosi hicho kuitwaa timu ya taifa ya Gabon pamoja na mchezaji moja kusajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili na klabu ya FC Rostov inayoshiriki Ligi Kuu Russia.

Pia Mbelgiji huyo amefundisha ukanda wa Afrika Mashariki akiiongoza AFC Leopards ya Kenya mwaka 2013 kwa kuinusuru kushuka daraja pamoja kufuzu kwa Kombe la Shirikisho Afrika 2014, pia aliwapa ubingwa wa Kombe la FKF President's Cup.

Januari 2014, alitimikia Rwanda na kujiungana Rayon Sport na kuisaidia kumaliza katika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Rwanda wakiwa wamekusanya pointi 34 kati ya 39 katika msimu wa 2013–14.

Mbali ya timu hizo pia amefundisha JS Kairouan ya Tunisia akisaidia kumaliza katika nafasi ya nane katika msimamo wa ligi ikiwa ni nafasi yake ya juu zaidi msimu wa 2013-14.

Alijiunga na Al-Nasr kabla ya kutimikia Sudan ambako alijiunga na Al-Merrikh na baadaye akitimukia Afrika Kusini.