VIDEO: Samatta afurahia kukutana na Msuva Ulaya ataka wengine waende

Muktasari:

  • Mbwana Samatta na Farid Mussa ni wachezaji pekee wa Taifa Stars wanaocheza soka ya kulipwa Ulaya wengine wanacheza barani Afrika.

Dar es Salaam. Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta anayecheza KRC Genk, ameshindwa kuficha furaha yake baada ya kukutana na Mtanzania mwenzake Simon Msuva barani Ulaya na kutaka wachezaji wengi wacheze soka barani humo.

Msuva anayeichezea Diffa el Jadida inayoshiriki Ligi Kuu Morocco, alikutana na Samatta jijini Istanbul, Uturuki wakiunganisha ndege ya kuja Tanzania.

Samatta alisema anafuraha kuona amekutana na Mtanzania mwenzake wakiwa wanakuja katika majukumu ya timu ya Taifa.

"Tumekutana wawili Ulaya tukiwa tunakuna kwenye majukumu ya timu ya Taifa, natamani sana tuwe tunakutana hata saba huko mbeleni," alisema.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Msuva aliyesema anatamani kuona wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje wanaoongezeka.

"Kama ambavyo kapteni kasema tu kwa sababu tunapokuwa na wachezaji wengi wanaocheza nje inakuwa na faida, hapa tumeongezeka kidogo, lakini tumeona taswira iliyopo," alisema.

Samatta na Msuva wamerejea nchini kwaajili ya kucheza mchezo wao dhidi ya Equatorial Guinea utakaopigwa Ijumaa kabla ya kuifuata Libya michezo ya kuwania kufuzu Afcon Cameroon 2021.